Na Derick Milton, Simiyu
Shirika la Haki Elimu kupitia mradi wake wa kusaidia wanafunzi wa kike kujitambua na kutimiza ndoto zao (GRTI) umewezesha watoto wa kike katika mkoa wa Simiyu kuanza kujitambua na kuweza kufikia ndoto zao.
Mradi huo unatekelezwa katika shule nane za wilaya za Itilima na Bariadi mkoani humo, mbali na kusaidia wasichana kujitambua, aidha umewezesha kuongeza ufaulu na kutoa stadi na ujuzi wa mambo mbalimbali.
Mratibu wa Mradi huo, Janeth Kato amesema kupitia mradi huo wamekuwa wakiwasaidia wasichana kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ambayo yanalenga kupunguza mdondoko wao katika elimu.
“Tumewasaidia mabinti wengi kupunguza mdondoko na watimize ndoto zao, mtu anakuwa na ndoto kwamba mimi nitakuwa nani…kila shule ambayo ipo kwenye mradi ina wasichana 15 na wavulana watano ambao tunawapa mafunzo kupitia maafisa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii na dawati la jinsia baadaye wanaenda wanawaelimisha wenzao,” amesema Kato.
Aidha, kupitia mafunzo hayo yamesaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa watoto, utoro pamoja na kusaidia ujenzi wa vyoo, huku akiiomba serikali kusaidia kuzitazua changamoto ambazo bado zinatajwa kuwakabili watoto wa kike ili kuwawezesha kuondokana nazo.
“Tunaweza kujivunia kupitia mradi huu, watoto wengi wa kike wameanza kujitambua kwa kiasi kikubwa, wamepewa mafunzo jinsi ya kupambana na changamoto wakiwa shuleni na nyumbani, kupambana na vikwazo vya kuweza kuwazuia watimize ndoto zao,” amesema Kato.
Amesema kuwa watoto wengi hasa wa kike katika mkoa wa Simiyu wamekuwa wakishindwa kutimiza ndoto zao, wakiwa shuleni na nyumbani kutokana na changamoto zilizopo, ambapo ameeleza kupitia mradi huo baadhi ya changamoto wameweza kuzitatua.
“Lakini pamoja na mafanikio bado changamoto ni nyingi kulingana na shule zetu zina wanafunzi wengi, vyumba vya madarasa havitoshi, matundu ya vyoo, bado kuna shule zinahitaji fensi, bado kuna shule zinahitaji mabweni, zingine zina mabweni vitanda hazina, hii ni fursa kwa wadau wengine pamoja na serikali kusaidia katika kuzitatua,” ameeleza Kato.
Kwa upande wake, Afisa kutoka Haki Elimu, Pius Makomelelo amesema changamoto katika suala la elimu kwa mtoto wa kike bado ni nyingi na haki elimu wataendelea kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema kuwa kupitia mradi huo, Haki elimu iliwezesha kuweka mazingira rafiki kwa watoto wa kike kwa kujenga vyoo safi na salama, ambavyo vimewazesha kuendelea na masomo muda wote hata wakiwa hedhi.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto wilayani Bariadi, Leila Mhando amezisisitiza shule nyingine kuona umuhimu wa kufikiwa na mradi huo ili kuwasaidia wasichana wengi zaidi huku akihimiza ushirikishwaji wa wazazi.
“Huu mradi moja kwa moja unatakiwa kwanza uhakikishe unafikia katika asilimia kubwa ya shule mbalimbali ili tuweze kuwasaidia wanafunzi wote kwa kiasi kikubwa, tunapochagua shule chache ina maana ni wachache wanafikiwa, je wale watoto wengine wa kike wanafikiwaje?,”amehoji Leila.
Baadhi ya walimu wa shule zilizopo kwenye mradi huo wamesema kuwa idadi kubwa ya watoto wa kike kwa sasa wanajitambua hasa wanapokuwa kwenye siku zao, ambapo ujitengenezea taulo za kike wao wenyewe na kuzitumia ipasavyo.
“Uko nyuma mtoto wa kike akiingia kwenye siku zake, anaamua kukaa nyumbani siku tatu hadi nne kila mwezi na masomo yanampita hivyo wengi kukataa tama, lakini kupitia mradi huu wanaweza kujihudumia wenyewe na wamejengewa vyoo rafiki,” amesema Mwl. Christina John.