28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

RUWASA Simiyu kukamilisha miradi yamaji kwa wakati

Na Samwel Mwanga, Simiyu

WAKALA wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) katika mkoa wa Simiyu watakamilisha miradi yote ya Maji inayotokana na fedha za Uviko-19.

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala amesema hayo juzi mbele ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi mara baada ya kutembelea miradi ya maji inayosimamiwa na Ruwasa katika mkoa huo.

Amesema kuwa wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu zinatekeleza miradi hiyo ya maji ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu kumtua Mama ndoo kichwani.

Mhandisi Majala amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo ya mkoa huo ikiwemo wilaya ya Meatu ambayo ina vyanzo vichache vya maji lakini kwa kutumia Utaalamu wao wameweza kutafuta maeneo ambayo maji yanapatikana ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

“Baadhi ya maeneo ya mkoa wa Simiyu yana ukame hususani wilaya ya Meatu  hivyo tunachokifanya tunaangalia maeneo ambayo tunaweza kupata chanzo cha maji na hivyo kuwapatia maji wananchi wetu,”amesema Mhandisi Majala.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha wanamaliza kwa wakati miradi hiyo ya maji wanawasimamia wakandarasi wote waliopewa kazi za ujenzi wa miradi ya maji ili wananchi waweze kunufaika na matunda ya serikali ya awamu ya sita iliyolenga kuwapatia maji safi na salama.

“Tunataka miradi hii tumalize kabla ya Aprili mwaka huu licha ya serikali kuweka muda wa Juni 30 mwaka huu kuwa miradi yote nchini nzima ya fedha za Uviko 19 inakamilika sisi tutatumia muda huo sasa kuona kama kuna maeneo ya kufanya marekebisho tunafanya kabla ya kukabidhi rasmi kwa serikali.

“Bado tunachangamoto ya upatikanaji wa mabomba ya kusambaza maji hivyo yule mfanyabiashara aliyepewa kazi hiyo tutambana ili kuhakikisha  tunamaliza kwa muda ambao tumepanga,” amesema.

Aidha, amewataka Wakandarasi wote waliopewa kazi ya ujenzi wa miradi hiyo katika mkoa wa Simiyu wanafanya kazi usiku na mchana huku akiwasisitiza Mameneja wa Ruwasa wa wilaya kusimamia kazi hizo kwa weledi wa hali ya juu.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mahundi aliwataka wafanyakazi wote wa Ruwasa katika mkoa huo kumpatia ushirikiano wa kutosha Meneja wa Ruwasa wa mkoa huo,Mhandisi Majala ili waweze kutimiza azima ya Rais Samia Suluhu kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama.

Pia alimpongeza Meneja huyo wa mkoa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuisimamia miradi hiyo ya maji na kumhakikishia kuwa atampatia ushirikiano wa kutosha ili aweze kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Simiyu wanapata maji kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani.

“Mhandisi Mariamu nikupongeze kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Maji iliyoko chini ya Ruwasa katika mkoa wa Simiyu na wale watendaji wote wa Ruwasa mpatieni ushirikiano ili mfanye kazi ambayo mnalipwa mishahara na serikali acheni maneno maneno tufanye kazi ya kuwapatia maji wananchi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles