Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
BENKI ya NMB imetunukiwa cheti cha kuthaminiwa kwa mchango uliofanikisha uzinduzi wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), iliyoasisiwa na mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi, huku benki hiyo kinara ikiahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za kukuza Uchumi wa Bluu unaochakatwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi.Â
NMB ilichangia pesa taslimu sambamba na ‘track suit’ na fulana ‘t-shirt’ zilizovaliwa na washiriki wa matembezi ya kilomita sita kuanzia Viwanja vya Butroz Ghali hadi Mao Zedong, ulikofanyika uzinduzi wa taasisi hiyo inayojihusisha na Maendeleo Endelevu ya Wanawake, Vijana na Watoto, lengo likiwa kuunga mkono juhudi za SMZ katika kufanikisha ustawi wa makundi hayo Kiuchumi, Kiafya na Kimaadili.
Cheti hicho kilitolewa na Mama Mwinyi na kupokelewa na Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali wa NMB, Vicky Bishubo, ambaye aliihakikishia ZMBF na Serikali ya Zanzibar, kuwa benki yake itaendelea kuwa mdau kiongozi na mtiifu katika kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo zenye nia ya kumkwamua Mzanzibar mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“NMB hatuko nyuma. Chini ya Rais Hussein Mwinyi kwa mfano, tumeuunga mkono harakati za Serikali yake kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Bluu na leo tunamsapoti Mama Mwinyi na Benki yetu itasimama naye hatua kwa hatua,” alisema Bishubo akikumbushia udhamini wa NMB katika Zanzibar International Marathon na uzinduzi wa Kadi za Utalii Zanzibar (ZATO), zinazotumiwa na Watalii visiwani humo.
Aidha, wakati Mama Mariam Mwinyi alipotembelea Banda la NMB kwenye uzinduzi huo katika Viwanja vya Mao, Bishubo alimsisitizia Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya ZMBF kuwa, kipaumbele chao ni mahusiano mema baina ya taasisi zao, ambayo yatachagiza ufanisi katika kufikia malengo ya kusapoti jitihada za Serikali inayohitaji nguvu za wadau katika kuharakisha maendeleo.