Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameonesha kukerwa na tabia ya baadhi ya watoto wa rika la kuwepo shule kuzurura ovyo mitaani ikiwemo maeneo ya vilabuni, masoko na minadani na kusema hataki kuona mtoto yeyote mwenye umri wa kuwa shule akiwa mtaani muda wa masomo.
Mtaka amemtaka kila mtu aliyefikia umri wa miaka 18 jijini Dodoma akimuona mtoto anazurura muda wa masomo aguswe na ahoji kwanini mtoto huyo yuko nje muda wa masomo na achukue hatua za kuhakikisha mtoto huyo anakuwepo shule na siyo kumtuma abebe mzigo sokoni.
Mtaka aliyasema hayo jijini hapa alipofanya ziara katika shule ya Msingi Mbabala akiongozana na Taasisi ya Nivishe nisome kwa ajili ya kutoa msaada wa sare za shule shuleni hapo.
“Watoto wote ni mali ya serikali, ndio maana nikasema sitaki kuona mwanafunzi anazurura mtaani wala mnadani pia nilitoa maagizo kuwa kila mzazi mwenye mtoto aliyefikia umri wa kuanza darasa la kwanza apelekwe shule na asiyefanya hivyo akamatwe akafanyekazi za usafi shuleni,”amesema Mtaka.
Pia ametoa maagizo kwa walimu kuwakumbusha wazazi wote wenye watoto waliokuwa kwenye madarasa ya mitihani ya Taifa wawape muda wa kujisomea na kuwapunguzia kazi za kufanya nyumbani ili wasome.
“Lakini diwani unapofanya mikutano yako, wasisitize wazazi watoto wasifanye kazi nyingi zaidi ya kusoma, wajiandae na mitihani,” amesema Mtaka.
Aidha, amewataka Afisa Elimu Sekondari na Msingi wa Jiji la Dodoma kutoa maagizo kwa Wakuu wa shule zote kuwajulisha wazazi kuwa lazima wawepo siku za kufunga shule ili waseme matatizo ya watoto wao na walimu wasema matatizo ya wanafunzi shuleni.
“Haya ni maelekezo yangu kila tunapoenda kufunga ni lazima kila shule wazazi waitwe na hata watoto waonyeshe vipaji vyao mbele ya wazazi wao kama ngoma lakini klabu za mazingira na Takukuru ni matarajio yangu nitakuja kuzungumza nao tuone yale ambayo yatatusaidia kujenga elimu yetu haiwezekanaimakao makuu hatupo kumi bora la nne, saba, kidato cha pili, cha nne na hata cha sita.
“Diwani wa Kata ya Mbabala simamia na usaidie kata hii wazazi watambue umuhimu wa elimu kwasababu hata hii migogoro mingine inasababishwa na elimu kuwa ndogo ndio maana wanauza ardhi kiholela na watu wamechukulia udhaifu wa watu kutokuwa na elimu kuwatapeli watu wa Dodoma kuuza viwanja mashamba holela,” amesema Mtaka.
Akizungumzia kampeni ya Nivishe nisome shuleni hapo, Mtaka amesema taasisi hiyo ya Nivishe nisome inalenga kutoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi 241 katika shule hiyo huku lengo likiwa ni kutoa sare 5,000 katika shule zote za Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mbabala, Pascazia Mayala amesema amepokea maagizo ya Mkuu huyo wa Mkoa nakwamba yatafika kwa wazazi na kusema hata yeye anakerwa na kuona watoto wanauza pombe vilabuni.
Naye Mkurugenzi wa Nivishe Nisome, Godfrey Kilimwomeshi, amesema wao kama taasisi ya vijana ambao wanatamani kuona kila kijana anasoma katika mazingira mazuri wamesema watahakikisha wanawawezesha wale wasio na uwezo kupata sare za shule.
“Sisi tunaamini hapa kwenye elimu ndio wanatoka viongozi wa Serikali, madaktari na watu wa kada mbalimbali, ndio maana tunafanya hivi na tunajiita nivishe nisome kwasababu tunamvalisha mwanafunzi ili asome kwa kujiamini,”amesema Kilimwomeshi.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Nathaniel Mwijumbe, ameahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kushukuru kwa msaada huo na kusema utawasaidia kuwatia moyo wanafunzi watakaonufaika na mpango huo.