Na Elizabeth Hombo, Dodoma
MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi (Chadema), amesema ana mpango wa kwenda mahakamani ili kupata ufafanuzi wa mahakama juu ya uhalali wa Bunge Maalumu la Katiba kuachana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya mwandishi wa habari, Said Kubenea chini ya wakili, Peter Kibatala kufungua kesi mahakamani kutaka Bunge la Katiba lisitishwe.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Arfi alisema kwa sasa anaendelea kushauriana na wanasheria wake endapo anastahili kufanya hivyo kwa kuwa tayari wengine wamefungua kesi inayofanana na hiyo.
“Kwa kuwa wabunge wa CCM wamedhamiria kuendelea na mchakato huu wa kuifanyia marekebisho Katiba ya sasa na kuachana na Rasimu ya Warioba na kwa vile hakuna namna ya kuwazuia kufanya hivi baada ya Ukawa kususa, ninakusudia kuchukua hatua za kisheria kwenda mahakamani ili kupata ufafanuzi wa mahakama juu ya uhalali wa Bunge Maalumu la Katiba kuachana na Rasimu ya Tume,” alisema Arfi.
Alisema kwa sasa kinachoendelea ndani ya Bunge hilo si kutengeneza Katiba mpya bali kufanya marekebisho makubwa ya Katiba iliyopo.
“Hili limewezekana kwa sababu wenzangu wa upinzani wamesusa, tungekuwepo wote ndani ya Bunge hili, lisingewezekana kwani tungepinga kwa nguvu zaidi na hata kuhakikisha Bunge haliendelei,” alisema.
Katika hatua nyingine, Arfi alisema bado yuko sahihi kuendelea na vikao vya Bunge hilo pamoja na kwamba wenzake wamesusa.
Alisema baada ya wenzake kususa sasa ni kama nyani amekabidhiwa shamba la mahindi lisilo na mlinzi.
“Ukweli ni kwamba, baada ya Bunge la Katiba kukataa rasimu ya Warioba ambayo ilipendekeza muundo wa Serikali tatu, kwa sasa haiwezekani tena kujadili rasimu ya tume hiyo.
“Kinachofanyika kwa sasa ni kuandika rasimu nyingine ili iendane na muundo wa Serikali mbili ambao ndio msimamo wa CCM, hii imekuwa rahisi kwa sababu hakuna upinzani wa kutosha kuzuia, wenzetu wa 201 wanaangalia zaidi masilahi ya makundi yao na muundo wa Serikali kwao si jambo linalowashughulisha sana,” alisema.
Alisema mambo makubwa ambayo yanaanzishwa ili kujaribu kuwashawishi Wazanzibari kuendelea na kuwa sehemu ya Muungano wa Serikali mbili, ni pamoja na kuanzishwa kwa makamu wa tatu wa rais.
Pamoja na hilo alisema kuna mambo mazuri ambayo yameingizwa kwenye rasimu ikiwemo haki za wakulima, wafugaji na wavuvi kumiliki ardhi, haki ya afya, chakula, majisafi na salama, haki ya hifadhi ya jamii na haki ya makazi.