28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

ISCEJIC yatoa mapendekezo kuhusu bima ya afya kwa wote

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

KAMATI ya Viongozi wa Dini kuhusu haki za kiuchumi na uadilifu wa uumbaji (ISCEJIC) imetoa mapendekezo saba kwa Serikali wakati ikiandaa kuleta muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa zote muhimu katika vituo vya afya ili kujenga imani kwa wanachama na watu wengine kuendelea kujiunga zaidi.

Kamati ya ISCEJIC inaundwa na viongozi kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Wakizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Januari 9, 2022 kuhusu umuhimu wa kupitishwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote nchini viongozi hao wameiomba serikali ihakikishe kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa zote muhimu katika vituo vya afya ili kujenga imani kwa wanachama na watu wengine kuendelea kujiunga zaidi.

Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Chesco Msaga ameyataja mapendekezo mengine ni serikali ijikite kwa nguvu katika kuelimisha jamii kuhusu dhana ya bima ili wajiunge zaidi.

“Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuratibu na kuelimisha watu kwa ajili ya kuandikisha watu. Serikali na wadau kama viongozi na taasisi za dini waunganishe nguvu za pamoja kuhamasisha watu kujiunga na bima ya afya kwa wote ili kuwa na wanachama wengi,”amesema Padri Msaga.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa TEC ameyataja mapendekezo mengine ni kuwa serikali lazima iweke kipaumbele endelevu cha kiwango cha fedha (matching founds) kitakachokuwa kinachangiwa katika kuendesha bima ya afya kwa wote.

“Serikali itafute na kutenga kwa mujibu wa sheria vyanzo maalum vya kodi kutoka katika maeneo yake mbalimbali. Serikali izingatie kuwa kuna Watanzania maskini kabisa, hivyo basi lazima itenge fedha za kuhakikisha wanalipiwa kiasi kikubwa cha bima kwani hawana uwezo wa kulipa bima kwa mwaka,” amesema Padri Msaga.

Pia, wameshauri sheria hiyo ipitishwe kwa sasa kwani muda umepita tangu majadiliano yake yaanza kujadiliwa, hivyo wanaomba ipitishwe au kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni ili iletwe kwa wadau na kisha ianze kujadiliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa ISCEJIC ambaye pia Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Hamis Mataka, amesema matokeo ya utafiti waliofanya ambao unalenga kutoa maoni ya uboreshaji wa huduma za afya nchini unaonesha kwa takriban muongo mmoja wastani wa bajeti kwa mwaka imekuwa ni asilimia 10 ya matumizi ya jumla.

Amesema mapendekezo ya viongozi wa dini kutokana na utafiti huo ni bajeti na kugharamia afya isichukuliwe kama gharama bali kama uwekezaji katika maendeleo ya mwanadamu.

“Pia, Watanzania milioni 15 sawa na asilimia 26.4 au kaya takribani milioni tatu ni maskini kabisa, hivyo basi serikali iwalipie bima zao ili wapate huduma za afya.

“Vilevile, iboreshe kitita cha huduma za bima kuwiana na malipo na bei za soko ili kuondoa changamoto katika utoaji wa huduma,” amesema Sheik Mataka.

Akitoa mapendekezo kwa waumini na jamii, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Canon Moses Matonya amehimiza waumini na watu wote kuunga mkono juhudi za serikali kupitisha sheria ya bima ya afya kwa wote  kwa kujiunga na bima hiyo kwa hiari pamoja na kushiriki kutoa maoni.

“Tunahimiza wananchi kushiriki katika kuchangia uimarishaji na ujenzi wa miundombinu  ya afya katika maeneo yao ili kuongeza wigo wa ufikiwaji na utoaji wa huduma bora za afya,”amesema Matonya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles