25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kafulila aagiza ukaguzi waliotafuna fedha za Afya

Na Derick Milton, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi maalumu kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za Afya ambavyo watumishi wake wanadaiwa kutafuna fedha za vituo hivyo.

Kafulila ametoa maagizo hayo leo, Jumatatu Novemba 8, wakati wa kikao kazi cha Kamati ya Afya Mkoa, ambacho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji sekta ya afya mkoani humo.

Kafulila amefikia uamuzi huo baada ya Mganga Mkuu wa mkoa, Dk. Boniphace Marwa kutoa taarifa za uwepo wa watumishi kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma za Afya hasa zahati kutafuna fedha za vituo hivyo.

Dk. Marwa amesema katika uchunguzi wao wamebaini baaadhi ya Waganga Wafawidhi kwenye zahanati mkoani humo, wamekuwa wakitoa huduma kwa wagonjwa na fedha za huduma wanazowatoza haziandikwi kwenye vitabu.

“Kuna baadhi ya zahanati, tumekuta mgonjwa amepewa huduma na amelipia huduma ile ambayo amepatiwa kama ambavyo inatakiwa, lakini zile fedha hazionekani, wengi wanazitumia zile pesa kwa matumizi yao wenyewe,” amesema Dk. Marwa.

Ameongeza kuwa hali hiyo imesababisha zahanati nyingi kwenye mkoa huo kupata changamoto kubwa ya ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba, kwani fedha kwa ajili ya kununua dawa zimekuwa zikiliwa na watumishi wake.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa mkoa ameta muda wa mwezi mmoja kufanyika kwa ukaguzi maalumu kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya hasa Zahati ili kubaini wale wote waliojihusisha na vitendo hivyo.

“Hatuwezi kuwa na watumishi wa namna hii, naagiza hapa ufanyike ukaguzi maalumu sehemu zote ndani ya mwezi mmoja nipate taarifa, wale wote ambao watabainika hatua kali zitachukuliwa,” amesema Kafulila.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa, amewasainisha mikataba ya utendaji kazi na usimamizi wa huduma za Afya wakuu wa Wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo.

Amesema kuwa kila baada ya miezi mitatu kitafanyika kikao kwa ajili ya kufanya tathimini juu ya utekelezaji wa mkataba huo, ambao ameeleza unakwenda kuboresha huduma za Afya mkoani humo.


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles