MBUNGE wa Viti Maalumu, Martha Mlata, amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Singida kuziba nafasi ya Mgana Msindai aliyetimkia Chadema mapema mwaka jana.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika mjini hapa jana, Katibu wa Halmashauri Kuu Oganizesheni ya CCM, Dk. Muhammad Seif Khatib, alimtangaza Mlata kuwa mshindi kwa kupata kura 433 (asilimia 50) huku wapinzani wake Mohamed Misanga akipata kura 261, Juma Kilimba kura 90 na Narumba Haje kura 69.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema wapiga kura 857 kati ya 946 walitakiwa kupiga ambako kura halali zilikua 852 na tatu zikiharibika.
Akitoa shukurani kwa wajumbe wa mkutano huo, Mlata alisema yupo tayari kuitumikia CCM kwa kuhakikisha inakuwa na mtandao imara katika mkoa huo.
“Ndugu zangu wana CCM naomba tuvunje makundi tusipovunja makundi hatutapata maendeleo hatimaye tutaanza kulaumiana.
“Mkinipa uenyekiti wa CCM nitakua kama kuku kukumbatia vifaranga vyake na kuwatafutia chakula… naahidi sintowaangusha,” alisema Mlata.