Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HALI ya afya ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, inaendelea vizuri baada ya kusumbuliwa na goti kwa siku za hivi karibuni.
Sitta mmoja wa mawaziri machachari ambao wamepata kuhudumu awamu zote nne zilizopita, alipelekwa Hospitali ya Agha Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya kukandwa goti ambalo limekuwa likimsumbua.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, mtoto wa waziri huyo, Benny Sitta, alisema baba yake anaendelea vizuri tofauti na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaumwa.
“Baba anaendelea vizuri, amekuwa akisumbuliwa na goti hivyo hulazimika kwenda Hospitali ya Agha Khan kukandwa kutokana na tatizo linalomsibu,” alisema Benny.
Mwaka jana, Sitta alikuwa miongoni mwa makada 40 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kugombea urais, huku akieleza anataka kulifanyia taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
Baada ya kuenguliwa na Kamati Kuu ya CCM, Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alitangaza kustaafu masuala ya siasa.
Sitta aliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe kirahisi uenyekiti wa Bunge la Katiba na kutangaza tena nia yake ya kutaka kurudi tena kuongoza Bunge la 11.
Lakini hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa angeenguliwa angefika hata mahakamani.
Mambo mengine aliyoahidi kuyafanya kama angechaguliwa kuwa rais, ni kusimamia Muungano, kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba mpya, kuweka mfumo wenye motisha kwa wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda, vita dhidi ya rushwa na kuiimarisha CCM kiuchumi.
Sitta alisema mikataba mibovu ya huduma na mauzo, ununuzi hewa, ununuzi uliojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa rushwa na hasa rushwa katika ajira, kumelisababisha taifa hasara kubwa.
Alisema hatua ya pili ya kupambana na rushwa ni kutunga sheria mpya kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa.