KESI ya kupinga matokeo ya jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa Novemba 2015 katika Mahakama Kuu kanda ya Tabora   itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia leo, mbele ya Jaji Dk. Wambura ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Mahakama Lushoto Tanga.
Kesi hiyoNa 2 ya mwaka 2015 yenye mvuto mkubwa wa siasa, itafanyika katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma kwa kipindi chote.
Habari zinasema  itakuwa kwenye mahakama ya wazi na hivyo kuvuta hisia na umma mkubwa wa wakazi wa Mkoa wa Kigoma.
Katika kesi hiyo, David Kafulila atawakilishwa na Wakili msomi, Profesa Abdallah Safari pamoja na Tundu Lissu wakisaidiwa na wakili mwenyeji wa Kigoma, Daniel Lumenyera.
Mbunge Hasna Mwilima  atawakilishwa na wakili  Kennedy Fungamtama pamoja na mawakili wa serikali wanaomwakilisha msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kama washtakiwa katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, mlalamikaji David Kafulila anaomba mahakama imtangaze mshindi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu No112 (c) kwa hoja kwamba yeye ndiye aliyepata kura nyingi kwa mujibu wa matokeo ya kila kituo kwenye fomu no 21B.
Anadai  kwamba msimamizi wa uchaguzi alimtangaza  Husna Mwilima kinyume na matokeo halisi.