27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ZEC yathibitisha Maalim Seif kutogombea urais

maalimNA KHELEF NASSOR, ZANZIBAR

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imethibitisha kutogombea urais kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad  katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.

Hatua hiyo ya ZEC inatokana na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha jana, ambayo ilivitaja vyama vinane vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo kwa ngazi ya urais huku CUF kikiondolewa katika orodha.

Taarifa hiyo  ya ZEC iliyosainiwa   na Mawenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, ilieleza ushiriki wa wagombea wanane wa nafasi ya urais wa   vyama vya  ADA-TADEA, ACT, ADC, CCK, AFP, SAU, TLP na CCM ikisema hao ndiyo waliothibitisha kushiriki baada ya kuandikiwa barua.

“Wagombea wanane wa nafasi ya urais kutoka vyama mbalimbali vya ADA-TADEA, ACT, ADC, CCK, AFP, SAU, TLP na CCM wamethibitisha kuwa watashiriki katika uchaguzi wa marudio. Utaratibu wa kuwapatia ulinzi wagombea hao umeshaanza,” alisema Jecha katika taarifa yake.

Uamuzi wa ZEC umetolewa siku chache baada ya CUF  kupitia Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, kusema kwamba kinaaendelea kusimamia msimamo wake wa kutorudi kwenye uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Machi 20  mwaka huu.

“Na tunasema haya hatutanii hata kidogo, CUF tumeandika barua kwa ZEC ya kujitoa na Maalim Seif ambaye ndiye alikuwa mgombea wetu, naye ameandika barua pia ya kuondolewa kwa jina lake kwenye karatasi ya ZEC.

“ZEC wamegoma kutoa jina lakini tunasena hapa hata Maalim achaguliwe kwa asilimia 99 hatokwenda kuapa ila ataendelea kusimamia uamuzi wa chama wa kutoutambua uchaguzi huo wa marudio,” alisema Mazrui.

Hata hivyo, ZEC    imesema kwamba bado inawatambua wagombea wote wa ngazi ya uwakilishi na udiwani ni halali na watashiriki katika uchaguzi huo wa marudio.

Katika taarifa hiyo ya ZEC,  Jecha, alisema umekwisha kufanyika uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo kwa wilaya zote 11 na sasa inaendelea na kazi ya usaili wa wasidizi wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote 54 ya Unguja na Pemba.

Jecha alisema kazi ya utayarishaji na upangaji wa vifaa vya kupigia kura kwa kila kituo cha upigaji kura imekamilika na vifaa vyote vya uendeshaji wa uchaguzi vimekwisha kupatikana kwa ajili ya uchaguzi huo.

Akizungumzia hatua ya ushiriki wa vyama mbalimbali katika uchaguzi huo, Jecha, alisema ZEC imefanya mawasiliano na vyama hivyo   na wagombea   kuwapa taarifa za maandalizi  ya uchaguzi huo.

Jecha alisema ameshngazwa na baadhi ya vyama kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari vikisema kuwa havitashiriki uchaguzi  na hivyo akavitaka  kuandika barua ya kutoshirki kwao.

Alikosoa barua zilizoandikwa na baadhi ya wagombea wengi hasa wa Chama cha Wananchi (CUF) wa ngazi ya Uwakilishi za kujitoa katika uchaguzi huo.

Alisema barua hizo  hazikufuata utaratibu wa  sheria   na kusisitiza kwamba bado ni wagombea halali katika uchaguzi huo wa marudio.

“Wagombea wengi na hasa wa CUF barua zao za kujitoa katika Ofisi za Tume za Wilaya na nakala Makao Makuu.

“Hakuna hata moja ambayo imefuata utaratibu wa  sheria, kwa mantiki hiyo bado tunawahesabu wagombea hao ni wagombea halali katika Uchaguzi Mkuu wa marejeo,” alisema Jecha katika taarifa yake.

Mwenyekiti huyo wa ZEC alisema kazi ya upangaji wa vifaa hivyo na kuvisambaza kuelekea kwenye ofisi za wilaya umeanza rasmi   Unguja na Pemba.

Alisema baada ya kukamilika rasmi, utaratibu wa kuvisafirisha katika wilaya husika utaandaliwa.

“Kwa ujumla maandalizi ya upigishaji wa kura ya marudio yanakwenda vizuri hadi hivi sasa, taarifa za maandalizi hayo zitakuwa zinatolewa kadiri siku zinavyoendelea,”  alisema.

Wakati Jecha akikitaja chama cha ACT-Wazalendo kuwa ni miongoni mwa vyama vilivyothibitisha kushiriki uchaguzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Juma Said Sanani, alisema kauli ya mwenyekiti huyo ni ya kujifurahisha tu.

Alisema wao kama chama tayari walikwisha kuiandikia ZEC uamuzi wao wa kutoshiriki kwao,   hivyo hatua ya Mwenyekiti huyo ni miongoni mwa mbinu za kutaka kuhalalisha uchaguzi huo ambao amesema kuwa umekwisha kufanyika.

“Nadhani Jecha anajifurahisha tu, sisi tulishawaeleza mapema na tumeshawaandikia barua, sasa uhalali wa kutulazimisha kushiriki ameupata wapi?” alihoji.

Alisema wanachama imara kutoka chama cha ACT-Wazalendo hawatashiriki kwenye uchaguzi huo ambao ameutaja kuwa ni batili.

Wakati huohuo,  Chama Cha AFP kimeahidi kushiriki katika uchaguzi wa marudio kama ulivyopangwa na ZEC na hivyo kimewataka wananchi kujitokeza kwa wingi  kushiriki katika uchaguzi huo.

Akizungumza na Mtanzania   jana, aliyekuwa mgombea wa chama hicho, Said Soud Daud, alisema chama chao kina kila sababu ya kushiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles