21.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli kuwatema wakuu wa mikoa 20

magufuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI Rais Dk. John Magufuli akitarajia kutangaza safu ya wakuu wa mikoa  na wilaya wapya, imebainika wapo zaidi ya 20 ambao watatemwa kutokana na sababu mbalimbali za utendaji.

Habari za kuaminika ambazo MTANZANIA ilizipata  Dar es Salaam jana, zilisema miongoni mwa  wakuu wa mikoa watakaoachwa wamo walioshindwa kutatua kero sugu zikiwamo za mapigano ya wakulima na migogoro ya ardhi ambayo kila kukicha imesababisha watu kadhaa kufariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pia wamo wakuu wa mikoa  ambao wanaweza kuachwa kutokana na kuwa na umri mkubwa na wanaonyesha wazi hawawezi kwendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano ambayo inatumia falsafa ya Hapa Kazi Tu.

Habari hizo zinasema wapo wakuu wa mikoa ambao wameshindwa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao kwa zaidi ya miaka 10 hadi 15 na kusababisha vurugu kuibuka kila wakati.Miongoni mwa mikoa iliyokithiri kwa migogoro hiyo ni Morogoro, Tanga na Manyara.

“Wapo wakuu wa mikoa  ambao hawatarudi kutokana na rekodi za matukio, wapo ambao kwenye maeneo yao   migogoro imedumu kwa zaidi ya miaka 10 na kuendelea, sasa viongozi wa aina hii unadhani watabaki kweli kwenye Serikali?

“Nakuhakikisha kule ambako kuna migogoro ya ardhi na mapigano ya kila siku wako hatarini kupoteza kibarua… unajua mheshimiwa kila siku anajiuliza hivi inakuwaje mkoa ambao una kamati za ulinzi na usalama za wilaya zinashindwa kuchukua hatua za kumaliza mapigano haya?

“Inawezekana zinafanya kazi kwa kutegeana au wengine wanakula kwa wafugaji na wakulima.

“Mpaka wiki iliyopita tumedokezwa kwamba ma-RC  20 hawatarudi katika nafasi zao kwa sababu wameshindwa kuonyesha kama wanaweza kuajibika ipasavyo,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo  hicho kilisema pia kuwa wengine ambao wako hatarini kutemwa ni wale wenye umri mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine wanapaswa kustaafu.

“Sikutajii ni mikoa gani kwa sababu hawa wanajulikana vizuri…pale kanda ya ziwa, nyanda za juu kusini na mikoa ya kaskazini ni maeneo  ambayo yataguswa mno.

“Unajua Dk. Magufuli na timu yake wanaangalia kwa kina mno  hata mikoa ya kanda ya magharibi nao hawako salama kwa sababu wapo wazee wetu ambao inaonekana wazi umefika wakati wa kupisha kizazi kingine ambacho kitasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,”kilisema chanzo chetu.

Kuhusu wakuu wa wilaya, chanzo hicho kilisema hakuna tofauti na wakuu wa mikoa kwa vile kila mmoja atapimwa kutokana na namna alivyoweza kusimamia majukumu ya Serikali tangu alipoteuliwa.

“Jambo moja kubwa ndugu yangu, hapa kila mmoja atapimwa kutokana na uwezo wake… nadhani unakumbua Rais mwenyewe alisema anawachunguza, tutarajie mabadiliko makubwa,” kilisema chanzo chetu.

Hivi karibu Rais Magufuli, alisema wakuu wa mikoa na wilaya wajiandae kuwajibika endapo maeneo wanayoongoza yatakuwa na ukosefu wa chakula na kusababisha wananchi kukumbwa na njaa wakati maeneo mengi ya nchi yamepata mvua ya kutosha. tangu mwishoni mwa mwaka  jana.

Mikoa ambayo imekuwa ikikumbwa   na njaa mara kwa mara  ni pamoja na Mara, Iringa, Dodoma,Tanga na Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles