32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe aagiza TARI kujenga kituo cha Utafiti wa mazao Kongwa

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kujenga kituo cha utafiti wa mazao ya Korosho, Ufuta na Karanga Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma kutokana na wakulima wa eneo hilo kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mbegu bora na za kisasa ya mazao hayo.

Pia ameagiza mkutano wa mwaka wa wadau wa Korosho kufanyika katika Wilaya hiyo pamoja na mtambo wa kubangua Korosho ujenge katika Wilaya hiyo ili kuwasaidia wakulima kuuuza zao hilo kwa bei ya juu tofauti na kuuza ikiwa ghafi.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 12, 2021 katika mkutano maalum wa wadau wa zao la Korosho, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, Naibu Waziri Bashe amesema Serikali itahakikisha inawasaidia wakulima za zao hilo kulima kisasa na kuuza korosho zao zikiwa zimebanguliwa kwani itawasaidia kuweza kupata fedha hivyo ameagiza Tari kujenga kituo cha utafiti kwa mazao ya Korosho,Ufuta na Karanga katika eneo hilo.

“Kituo cha ubanguaji kitajengwa hapa,hii kazi ianze, Tari pia mnatakiwa kujenga kituo cha utafiti wa mazao ya Korosho,Ufuta na Karanga,” amesema Bashe.

Naibu Waziri huyo pia amewataka wakulima za zao la Korosho kulima mazao zaidi ya mawili katika mashamba ya Mikorosho ili kuweza kupata kipato mwaka mzima.

Aidha, Bashe amesema kutokana na mwamko wa ulimaji wa zao la Korosho katika Wilaya hiyo amewaagiza Maafisa Ugani kuweka kalenda katika ofisi zao ili mkulima aweze kujua miezi ya kupanda,kuweka dawa, kupalilia ni ipi huku akidai Serikali inaangalia namna bora ya kuwapatia ruzuku.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge na Mbunge wa Kongwa ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Job Ndugai amesema zao la Korosho ni mkombozi katika Wilaya hiyo ambapo amedai wao wanachohitaji kwa sasa ni kiwanda cha kubangua Korosho katika Wilaya hiyo.

Amesema wakulima ni lazima waingie katika ulimaji wa kisasa ikiwa ni pamoja na kuwa na simu janga ili kuweza kutatuliwa matatizo yao kwa wakati hususani miti inapokubwa na magonjwa.

“Simu janja ni muhimu dunia ndio iko huko,unataka hutaki simu janja ni muhimu.Tumejipanga sasa Kusini mtupishe na iko siku tutawapa challenge,”amesema Spika Ndugai.

Naye, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko kutoka kampuni ya kusambaza viwatilifu ya Bens Agrostar Co Ltd,Patrick Mwalunenge amesema wamekuwa wakitoa viwatilifu bora kwa wakulima za zao hilo ambapo kwa sasa wamejipanga kuanza kufunga mabomba katika mashamba ya wakulima ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Amewashauri wakulima kuwa na utaratibu kutibu magonjwa kwa wakati kwa kutumia dawa mbalimbali ambazo wanazo kwani mche wa mkorosho unahitaji matunzo ili uje utoa korosho bora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa,Remidius Mwema amesema wamejipanga kuhakikisha zao la Korosho linakuwa la kimkakati na linawasaidia wakulima kujiondoa katika lindi la umaskini.

Naye,Afisa Kilimo wa Mkoa wa Dodoma,Benard Abraham  amesema mwelekeo wa Mkoa wa Dodoma ni Korosho zisiuzwe ghafi na badala yake kila mkulima anatakiwa kubangua ili kujiongezea kipato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles