Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mwanamke anapaswa kuheshimiwa katika jamii kutokana na majukumu makubwa aliyopewa na Mwenyezi Mungu ya kubeba ujauzito, kujifungua na kulea mtoto mpaka anakuwa mkubwa.
Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 28, 2021 wakati akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Anglikana Tanzania yaliyofanyika jijini Dodoma.
“Miaka 50 tunayoadhimisha leo ni tangu Kanisa la Anglikana Tanzania lipate usajili lakini kwa ujumla limekuwepo nchini kwa takribani miaka 176 na lilianza kufanya kazi Tanga, Mpwapwa na kule kwetu Zanzibar.
“Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa, kuwainua wanawake, kijamii, kiuchumi na kisiasa, kupambana na ukatili dhidi ya kejeli, dharau na manyanyaso dhidi ya wanawake na watoto, tunafanya hivi sio kwa sababu mimi ni mwanamke pia la! hasha.
“Tunapozaliwa wote tunatoka sawa, kuna mwanaume amekuja na kibaka kinasema huyu ana akili zaidi, kuna shape ya kichwa inayosema huyu akiwa na kichwa hiki ana akili nyingi zaidi, kuna mwanaume anayezaliwa na nguo zake, hakuna.
“Mimi ninabeba mimba najifungua wewe huwezi, Mungu amenipa heshima ya kuleta viumbe wengine duniani, unachokifanya wewe (mwanaume) ni kunichangia tu mbegu yako mengine yote nafanya mwenyewe, ndiyo maana makabila mengine mtoto ni wa Mama.
“Mzigo alionipa Mungu ni mkubwa na ni heshima, lazima niheshimiwe, nyote nimewaleta mimi, nimewakuza, ukiumwa ni mimi, shibe yako ni mimi, raha yako ni mimi, sasa unaponiona ni mtu wa daraja la pili sikuelewi.
“Wanawake ni zaidi ya 50% kwenye nchi hii mkituacha nyuma nchi itaendelea lini na malengo ya kimataifa yanatuambia mtu asiachwe nyuma, sasa mnapowadogosha wanawake, mkawanyima haki zao, mkawanyang’anya ardhi zao maendeleo yatakuja lini,” amesema Rais Samia.
Aidha amesema Serikali itaendelea kuwapatia Mikopo ya Elimu ya Juu wanafunzi wa Vyuo Vikuu vinavyomilikiwa na Kanisa, kutoa vifaa tiba na vitendanishi, kuajiri na kulipa mishahara watumishi wa afya kwenye vituo na hospitali tunazoingia makubaliano.