Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kutoa elimu kwa waumini juu ya umuhimu wa kupata chanjo ya uviko -19 pamoja na kushiriki katika sensa inayotarajiwa kuanza mwaka 2022.
Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 28, 2021 wakati akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Aghlikana Tanzania yaliyofanyika jijini Dodoma.
“Ukweli ni kwamba chanjo zinapunguza vifo lakini pia inapunguza makali ya maumivu ya ugonjwa wa corona, wale ambao hamjawahi kupata maumivu ya lile gonjwa hamuwezi kuelewa lakini wale ambao yameshawafika wanaelewa.
“Niwaombe viongozi wa dini muwaelimishi waumini ili wakubali kupata chanjo ya corona, tumesema sio lazima kuchanja lakini wengine hawajui akichanja anapata nini na asipofanya hivyo anakosa nini.
“Nashukuru na ninawapongeza vijana waliojaribu kuja na chanjo, wakiibadilisha ikawa maji ikaweza kuingizwa kwenye bomba la sindano na kuchanja, tutaipeleka kwenye taasisi za Kimataifa ili ifanyiwe uchunguzi, ikithibitishwa watu wataitamani zaidi sababu imetengenezwa hapa na wenzetu na watachanja. Chanjo ni kinga tu,” amesema Rais Samia.