28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WaterAid Afrika yataka maji kuwa sera kuu ya hali ya hewa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakati Wiki ya Hali ya Hewa Afrika 2021 ikianza Jumapili hii, WaterAid Afrika imetaka hatua za haraka zichukuliwe na kutengwa fedha za kufanya maji kuwa sera kuu ya hali ya hewa barani Afrika.

Hiyo imetokana na mabadiliko ya hali ya hewa kutishia usambazaji wa maji kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi barani Afrika.

Wiki ya Hali ya Hewa barani Afrika inayotarajia kuanza leo Septemba 26-29, imeandaliwa na Uganda ikishirikiana na UN ikiwa ni maandalizi ya nchi za kiafrika kuelekeza mkutano wa hali ya hewa wa mwaka 2021 wa Umoja wa Mataifa (COP26) nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa WaterAid Afrika, malengo na mpango yao ni kuhakikisha wajumbe wa watakaohudhuria Wiki ya Hali ya Hewa Afrika 2021, wanajumuisha mahitaji yao katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa (COP26) utakaofanyika Novemba mwaka huu nchini Uingereza.

Inaeleza kuwa ripoti ya mwaka huu ya jopo la Serikali za Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) inaonyesha uhusiano kati ya mabadiliko ya hali ya hewa na maji.

WaterAid imeonya kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na athari hatarishi za mabadiliko ya hali ya hewa, ambazo zinahusiana na upatikanaji wa maji, mafuriko, ukame, mifumo ya hali ya hewa isiyotabirika na chumvi kutoka baharini zinazoongezeka.

Mkurugenzi wa WaterAid Kanda ya Afrika Mashariki, Olutayo Bankole-Bolawole anasema: “Tunahitaji hatua za haraka kuhakikisha kuwa walio katika mazingira magumu zaidi barani Afrika wanaweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kwa kuzingatia uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya hali ya hewa na maji, inamaanisha kuwa kila mtu lazima awe na chanzo cha kuaminika na endelevu cha maji safi na upatikanaji wa choo kilicho safi, salama na kinachostahimili hali ya hewa,” amesema Bankole-Bolawole.

Anafafanua kuwa kufikia mipango hiyo inahitaji kutumia kiasi kikubwa cha fedha kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amefafanua kuwa kwa sasa, ni 5% ya ufadhili wa hali ya hewa unaotumika kusaidia nchi kukabiliana na hali ya hewa inayobadilika, fedha ambazo hazilengi jamii zilizo hatarini zaidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kiwango hiki cha fedha hakiwezi kabisa kutatua shida inayozidi kuongezeka, ni muhimu kuanza mipango ya kurekebisha sasa ili kujenga uimara kwa siku zijazo,” anasema Bankole-Bolawole.

Anasema Wiki ya Hali ya Hewa barani Afrika ni fursa kwa serikali na wafadhili na taasisi za kitaifa katika kukabiliana na hali ya hewa na kujadili ufadhili unaohitajika kufanya mabadiliko ya hali ya hewa kuwa endelevu.

“Tunataka serikali zote kushughulikia haraka athari za tatizo la hali ya hewa na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi ni sehemu ya kimkakati ya mikakati yao ya kitaifa ya kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles