Na Derick Milton, Bariadi
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu (BARUWASA) imedai kuelemewa na uhitaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Mji wa Bariadi kutokana na uhitaji kuwa mkubwa kuliko uzalishaji wake.
Meneja wa BARUWASA, Musalila Masatu, amesema hayo jana mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, David Kafulila, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Stendi ya zamani mjini Bariadi.
Kabla ya meneja huyo kueleza hayo katika mkutano huo, wananchi walilalamika mbele ya mkuu huyo wa mkoa juu ya kutopatikana kwa huduma ya maji katika maeneo yao kwa zaidi ya siku tatu hadi nne.
Mmoja wa wananchi hao, Mariamu Majiku, amesema kuwa huduma ya maji imekuwa kero kwani katika mtaa wa sima ambako anaishi, wamekuwa wakipata maji mara moja kwa wiki hali ambayo inawafanya kuangaika na huduma hiyo.
“Sisi wakazi wa mtaa wa Sima tunaangaika na huduma ya maji, sasa hivi tunapata mara moja kwa wiki, hatujui tatizo ni nini? Tunaomba Mkuu wa Mkoa utusaidia maji hakuna mtaani kwetu, amesema Mariamu.
Baada ya malalamiko hayo Mkuu wa Mkoa alimtaka meneja huyo ufafanua, ambapo Masatu alieleza kuwa changamoto wanayoipata ni uwezo wa mamlaka hiyo kutoa huduma kwa wananchi wote wa mji wa Bariadi.
Masatu ameeleza kuwa mahitaji ya wakazi wa mji huo ya maji kwa siku ni lita milioni saba na mamlaka hiyo uwezo wake kwa sasa wanazalisha lita milioni mbili sawa na asilimia 35 ya mahitaji.
“Mamlaka vyanzo vyake vya maji ni visima virefu ambavyo ni zaidi ya 20, lakini visima hivi ukifika wakati wa kiangazi kama sasa vinapungua maji, hivyo uhitaji unakubwa mkubwa kuliko uzalishaji,” ameeleza Masatu.
Aidha Meneja huyo amesema kuwa kutokana na hali hiyo mamlaka imekuwa ikitoa maji kwa mgao, ili kuweza kuwahudumia wananchi wote, ambapo alieleza katika mtaa wa sima mamlaka hiyo itafanya ufuatiliaji kujua tatizo ni nini kwani wamekuwa wakitoa maji zaidi ya mara tatu kwa wiki.
Katika mkutano huo Kafulila alipiga marufuku magari madogo (mchomoko) kuingia mjini kuchukua au kushusha abiria na badala yake waishie stendi kuu ya magari yote makubwa na madogo Somanda.
Aidha amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya bilioni 18 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mjini na vijijini zilizoko chini ya Tarura, ambapo aliwataka watalaamu kusimamia fedha hizo kwa uadilifu.