24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tanga kuzalisha katani tani 60,000

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema mkoa huo umejipanga kufufua zao la mkonge kwa kasi huku akiweka matarajio ya kuzalisha tani 60,000 za katani inayotokana na zao hilo kwa mwaka.

Amesema miaka 50-55 iliyopita, Tanga ilikuwa inazalisha zaidi ya tani 1,500,000 za katani ambapo kwa sasa imeshuka hadi  kufikia tani 20,000.

Malima amesema hayo jijini Tanga jana wakati akizungumza na Wanachama na Wadau wa Chama cha Mkonge Tanzania (SAT).

“Lengo la Mkoa wa Tanga ni kufikia tani 60,000 ndivyo tulivyojiwekea mimi, halmashauri na wadau wangu kwa ujumla. Yaani kabla hatujaenda kwenye uchaguzi mkuu ujao tunataka Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) asimame kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) awaambie watu wa Tanga kwamba kwenye tani hizo 100,000 ambazo zimelimwa kitaifa, tani 60,000 zimetoka kwenye Mkoa wa Tanga kwa sababu tani 60,000 ni kama sh bilioni mbili ambazo ukiongeza kwenye kipato cha mkoa ni fedha nyingi sana.

“Kwa hiyo hayo ndiyo matarajio yetu kwa sababu unajua kuna kutaka na kufanya, tunaweza tukataka kwamba tunataka tufikishe tani 60,000 ifikapo miaka mitano ijayo lakini uipangie mikakati kwa hiyo mikakati tumejipangia na nafasi ya kila mmoja kama Serikali kuu, serikali ya mkoa, halmashauri na wadau kwa maana ya Wizara ya Kilimo katika kufikia malengo hayo,” amesema Malima.

Aidha, Malima amesema katika malengo hayo  wamegawana majukumu kwenye uzalishaji huo ambapo wakulima wadogo na wa kati Mkoa wa Tanga wanatakiwa kuzalisha tani 10,000-15,00 na wakubwa wazalishe tani 30,000-40,000.

Pamoja na mambo mengine, Malima amesema katika mazungumzo yao na wanachama hao wa SAT, wamekubaliana na kupeana maelekezo mbalimbali yakiwamo yale yanayochangia kwenye mafanikio na kudumaza zao la mkonge.

“Katika kudumaza wamelalamikia kodi mbalimbali, utaratibu wa bandarini kwamba watu wanatoa mkonge Tanga kupeleka Dar es Salaam na kusafirisha nje ya nchi  kwa sababu Bandari ya Tanga inatoza kodi kubwa zaidi hatua inayoongeza bei ya mkonge na kuufanya mkonge wa Tanga kutokuwa na ushindani dhidi ya mkonge mwingine,” amesema Malima.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saad Kambona amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kutekeleza malengo ya serikali kuongeza uzalishaji kufikia tani 120,000.

“Sisi kama Bodi ya Mkonge katika kufanikidha hayo tumeshatengeneza mkakati kwa kuwatembelea wakulima wakubwa kupanga mikakati ya pamoja katika uendelezaji wa mashamba kwa mwaka huu hadi 2026 kwamba waongeze uzalishaji, watapanda eka ngapi, mkonge walio nao, wa kuvuna ni eka ngapi ambao bado mdogo unategemea kuvunwa mwaka mmoja au miwili baadaye ni eka ngapi, kwa hiyo tunayo mipango ya pamoja,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles