NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikipoteza Sh bilioni 11 kila mwaka kutoka katika vyanzo vya mapato vya mabango makubwa ya matangazo.
Upotevu huo umegundulika baada ya manispaa hiyo kufanya utafiti kupitia kampuni tatu binafsi na kubainika ukusanyaji mdogo wa mapato kupitia ushuru wa mabango hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, alisema upotevu wa fedha hizo ulikuwa ukitokea kila mwaka kupitia makampuni 12 ya matangazo makubwa ambayo yamekuwa yakishirikiana na watumishi wa manispaa hiyo.
Alisema tangu alipoingia katika uongozi wa manispaa hiyo, wamebaini udanganyifu mkubwa uliokuwa unafanywa na walipaji wa ushuru jambo lililosababisha kufanya utafiti.
“Hapo awali manispaa kupitia vyanzo vyake vya mapato kupitia ushuru wa mabango tulikuwa tukikusanya shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka, lakini tulikuwa tukilaumiwa kwa kukusanya kiasi kidogo, ila kwa sasa tumegundua katika ukusanyaji huo hata robo tulikuwa hatufikii.
“Hayo mabango mnayoyaona barabarani yalikuwa na udanganyifu wa vipimo pamoja na idadi kwa kila kampuni, tumepitia mabango yote katika manispaa hii na idadi yote tunayo na tumeyapima upana pamoja na urefu, tumegundua tulikuwa tukipoteza zaidi ya bilioni 11.5 kwa mabango makubwa na kwa makampuni ya mabango madogo tulikuwa tunapoteza milioni 662,” alisema Meya Jacob.
Alisema walipaji wa ushuru wa mabango walikuwa wanaidanganya halmashauri kuwa kwa mwaka mmoja badala ya kupata Sh bilioni 13 wanapata Sh bilioni 2.5.
Meya Jacob alisema kutokana na uthibitisho wa takwimu walizonazo, wamebaini Kampuni ya OutDoor A1 inadaiwa zaidi ya bilioni moja kwa kuwa na mabango 74 katika manispaa hiyo, huku yenyewe ikilipia ushuru mabango 34 ambayo ilikuwa ikiyalipia Sh milioni 500 kwa mwaka, huku kukiwa na upotevu wa Sh milioni 894.
Aliyataja makampuni mengine ambayo yanatakiwa kuilipa halmashauri hiyo ni Masoko Agency inayodiwa Sh milioni 200, Continental inayodaiwa Sh milioni 825, Tan Outdoor Sh milioni 309, Block Line Media Sh milioni 452, Spark All Sh milioni 161 na Global System Sh milioni 116.
Mengine ni Scop Media Sh milioni 17, Label Promotion Sh milioni 111, Ashtone Media Sh milioni 218 na Platinum Media Sh bilioni 1.119.
“Kutokana na udanganyifu uliofanywa na makampuni hayo, tunayapa siku saba yawe yameshalipa fedha hizo, bila hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kushusha mabango yao yote katika manispaa hii,” alisema.
Meya Jacob alisema fedha zitakazopatikana zitatumika katika utoaji wa elimu bure, ujenzi wa zahanati pamoja na barabara katika manispaa hiyo.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2015-16 manispaa hiyo inatarajia kukusanya Sh bilioni 46 kutoka katika vyanzo 46 ambapo hadi sasa kupitia vyanzo sita vikubwa wameshakusanya zaidi ya Sh bilioni 35 ambazo ni sawa na asilimia 76.