Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemkamata  mwalimu wa Shule ya Sekondari Sungwizi na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Akisoma mashtaka dhidi ya mtuhumiwa huyo, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru wilayani hapa,  Aidan Samali, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Igunga, Leonard Nkola, alidai kwamba mnamo Julai  mwaka 2010 na Desemba mwaka 2011 katika Shule ya Sekondari Sungwizi, mshtakiwa Sostenes Jiboko (38),  alitumia vibaya madaraka yake.
Mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo akiwa Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sungwizi  alitumia mamlaka yake vibaya na kusajili mwanafunzi ambaye jina lake limehifadhiwa ili aweze kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili kinyume cha utaratibu.
Aidha mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria namba 3 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Baada ya mwendesha mashitaka kumsomea mashtaka mshtakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo na kesi yake kuahirishwa hadi Februari 29, mwaka huu itakapotajwa tena na mshatakiwa yupo nje kwa dhamana.