32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nyumbani kumenoga!

Ronaldo, Lukaku na wengine waliorudi klabu za zamani

DIRISHA la usajili la kiangazi litafungwa wiki ijayo, Agosti 31, lakini yapo mengi yaliyojitokeza tangu lilipofunguliwa rasmi miezi miwili iliyopita (Juni 9, 2021). Kubwa linaloweza kukumbukwa ni tukio la Lionel Messi kutua PSG akitokea Barcelona. Ameicha klabu aliyoitumikia tangu akiwa mdogo.

Kwa upande mwingine, dirisha hili la usajili wa kiangazi lilikuwa na taswira nyingine ya kuvutia mbele ya wapenzi wa soka. Ni kitendo cha baadhi ya mastaa kurejea kwenye klabu walizoziacha miaka mingi iliyopita. Ni aidha walishindwa kupata namba wakati huo, au waling’ara na kujikuta wakisajiliwa na klabu hizo.

Ashley Young (Aston Villa)

Licha ya kuwa zao la Watford, Ashley Young alipata jina kubwa England akiwa na ‘uzi’ wa Aston Villa, ambapo msimu wake wa pili tu akiwa na timu hiyo alitwaa mara mbili tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi.

Baada ya kuichezea kwa mafanikio Manchester United, Young mwenye umri wa miaka 36 alitimkia Italia kujiunga na Inter Milan. Kwa sasa, ameikacha Inter na kurudi Aston Villa.

Cristiano Ronaldo (Man United)

Imekuwa habari kubwa ukiacha ile ya Messi kwenda PSG akitokea Barca. Ronaldo (36), alisajiliwa na Man United mwaka 2003, kisha akanaswa na Real Madrid miaka sita baadaye. Tofauti na Lukaku, Ronaldo hakufeli Man United, bali Real Madrid walimchukua kwa kuvunja rekodi ya usajili duniani.

Tofauti na mwaka 2009, kwa sasa Ronaldo ameimarika zaidi. Mataji ya Ligi Kuu zote alizokwenda, kwa maana ya La Liga na Serie A. Pia, ameongeza tuzo nne za Ballon d’Or ukiacha ile moja aliyochukua akiwa Old Trafford.

Douglas Costa (Gremio)

Baada ya miaka mitano akiwa na Shakhtar Donetsk, kisha miaka sita akizichezea Bayern Munich na Juventus, Costa mwenye umri wa miaka 30 amerejea Brazil kujiunga na timu yake ya zamani, Gremio.

Hata hivyo, Gremio wamemrudisha nyumbani kwa mkopo akitarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu ujao.

Eric Garcia (Barcelona)

Garcia (20), beki wa kati anayesifika kwa utulivu wake awapo na mpira mguuni. Alitokea La Masia na sasa amerejea Barca akitokea jijini Manchester, England, alikokuwa akiichezea Man City iliyomsajili mwaka 2017.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola, alimbembeleza vilivyo ili asaini mkataba mpya lakini dogo alisisitiza kuwa anataka kwenda kuitumikia Barca. Aliondoka bure Etihad kwani mkataba wake ulishakwisha.

Gianluigi Buffon (Parma)

Akiwa na umri wa miaka 43 kwa sasa, Buffon amemaliza miaka 19 ya kulilinda lango la Juventus na kurudi Parma. Ndiyo timu iliyoibua uwezo wake mkubwa wa kuokoa michomo. Alipotua Juve mwaka 2001, Muitalia huyo aliweka rekodi kubwa mbili.

Mosi, alikuwa ndiye kipa ghali zaidi kwenye historia ya soka. Pili, ndiye aliyekuwa mchezaji wa bei mbaya zaidi kuwahi kununuliwa na Juve. Hata hivyo, rekodi zote hizo zimeshavunjwa kwa nyakati tofauti.

Kevin-Prince Boateng (Hertha Berlin)

Boateng (34), amerejea Hertha Berlin iliyoibua kipaji chake. Baada ya kutamba Ulaya akiwa na Tottenham, Borussia Dortmund, AC Milan na Barcelona, timu yake ya mwisho ilikuwa Monza ya Daraja la Pili Italia (Serie B), ambayo ameachana nayo miezi mitatu iliyopita.

Romelu Lukaku (Chelsea)

Alipotua Chelsea mwaka Chelsea, Lukaku alishindwa kupata namba mbele ya mpachikaji mabao hatari wa wakati huo, Didier Drogba. Akapelekwa kwa mkopo West Brom na Everton iliyomnunua moja kwa moja.

Baadaye aliibukia Man United na kufeli chini ya kocha Jose Mourinho. Ndipo alipokimbilia Inter Milan ambako amefanya vizuri na sasa anarudi Chelsea akiwa na umri wa miaka 28.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles