25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

‘Someni kwa bidii, tunawategemea’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, amewataka wanafunzi wenye ulemavu kusoma kwa bidii kwani wanategemewa katika ujenzi wa taifa.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, akisalimiana na mmoja wa wanafunzi wenye ulemavu anayesoma katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.

Akizungumza leo Julai 29, wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, amesema Serikali inawajali watu wenye ulemavu ndiyo maana imekuwa ikiandaa na kusimamia programu mbalimbali na kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanasoma vizuri.

Misaada hiyo iliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) inajumuisha kompyuta moja, karatasi maalumu, vibao na fimbo kwa ajili ya wanafunzi wasioona, taulo za kike, vifaa vya kuzima moto, vifaa vya usafi na sanduku la huduma ya kwanza.

“Ninyi ni wa thamani sana na mnao uwezo mkubwa, tunawategemea na tunawahitaji katika ujenzi wa taifa, mnaweza kuwa kama Samia (Rais) au kuwa kama mimi hivyo, someni kwa bidii,” amesema Nderiananga.

Aidha amewapongeza OSHA kwa kuguswa na changamoto za watu wenye ulemavu na kuziomba taasisi zingine na mtu mmoja mmoja kuiga mfano huo.

Naye Mtendaji Mkuu OSHA, Khadija Mwenda, amesema misaada hiyo wameitoa kupitia sera yao ya kusaidia jamii ambapo kila mwaka huelekeza faida wanayoipata katika sekta za elimu, afya na miundombinu.

“Kundi la watu wenye ulemavu linahitaji mwitikio wa kijamii na asasi mbalimbali kwa sababu tunataka mwisho wa siku waweze kujitegemea na kusaidia familia zao. Tutaendelea kusaidia kuhakikisha tunatatua changamoto mbalimbali zilizopo,” amesema Mwenda.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Christina Wambura, amesema ina wanafunzi 584 na kati yao 114 wana ulemavu wa aina mbalimbali.

Wanafunzi wenye ulemavu na idadi yao kwenye mabano ni wasioona (47), viziwi wasioona (10) na ulemavu wa akili (57).

“Shule yetu imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma katika mitihani ya kitaifa, mwaka 2020 wanafunzi wote wa darasa la saba walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari,” amesema Mwalimu Wambura.

Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto za kukosekana kwa ukuta wa kutenganisha mabweni ya wanafunzi na nyumba za walimu, usafiri wa kuwapeleka wanafunzi hospitali, dawa muhimu katika zahanati yao na madawati.

Mmoja wa wanafunzi wenye ulemavu wa akili, Abdulrahim Jumanne, ameshukuru kwa msaada huo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles