Na Winfrida Mtoi
Uongozi wa Klabu ya Simba umeachana na Haji Manara na kumteua Ezekiel Kamwaga kuwa Kaimu wa Idara ya Habari na Mawasiliano kwa muda wa miezi miwili.
Hivi karibuni Manara aliingia katika mgogoro na uongozi wa klabu hiyo, akilalamikia kutotendewa haki na kushutumiwa kuihujumu timu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo leo Julai 28, 2021, imeridhia matakwa ya Manara ya kutoendelea kuhudumu katika nafasi ya usemaji wa klabu , hivyo kumshukuru kwa maneno aliyoyatumia kuwaaga Wanasimba.
“Bodi inamshukuru kwa maneno aliyoyatumia kuwaaga Wanasimba katika kundi la viongozi wa Simba (Simba HQ) na kwa kazi aliyoifanyia klabu katika kipindi alichishika nafasi hiyo na tunamtakia kila la kheri,” imesema taarifa hiyo.
Aidha bodi hiyo imesema Kamwaga atashiriki katika maboresho ya muundo na utendaji wa idara ya Habari na baada ya maboresho kukamilika, itatangaza fursa mbalimbali za ajira.