26.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 24, 2021

Mwalimu mkuu akimbia nyumba kisa nyoka

Na Allan Vicent, Kaliua

MWALIMU Mkuu wa shule ya sekondari ya Dkt John Pombe Magufuli iliyoko katika kata ya Kamsekwa,Tarafa ya Igagala wilayani Kaliua mkoani Tabora, amekimbia nyumba aliyojengewa na shule kwa hofu ya nyoka aina ya koboko.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kamsekwa Ramadhan Juma mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kaliua ,Aloyce Kwezi alipokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mwenyekiti amemweleza Mbunge na Kamati nzima ya Mfuko wa Jimbo kuwa nyumba hiyo licha ya kukamilika tangu mwaka 2015 haikaliwi na mtu yeyote kwa sababu ya nyoka huyo aliyeko ndani, Mkuu wa shule alilazimika kwenda kupanga kwingine.

Amebainisha kuwa licha ya yeye mwenyewe kutomwona lakini waliomuona walieleza kuwa ni nyoka aina ya koboko na tangu aonekane katika nyumba hiyo Mwalimu Mkuu hakuingia tena hadi leo.

‘Tulileta wazee wa kimila wakafanya tambiko baadae akaja mchungaji kuombea nyumba hiyo lakini wanaogopa kwenda kufungua mlango ili kujiridhisha kama bado yupo au alishaondoka,  hofu bado ni kubwa, tunahitaji msaada’, alisema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Leonard Assenga, amesema walimu na wanafunzi  wana hofu kubwa na nyoka huyo kwa kuwa hadi sasa hawana uhakika kama ameshaondoka au vipi kuwa anaogopa kuingia humo kwa usalama wake.

Amefafanua kuwa hakuna madhara yoyote yaliyosababishwa na nyoka huyo ila hofu bado ni kubwa miongoni mwa walimu na wanafunzi, hivyo akaomba juhudi zifanyike ili kumwondoa na kumwezesha kurudi katika nyumba yake.

Mwanafunzi Joseph Jackson ambaye ni kaka mkuu wa shule hiyo amesema hawana raha na wanashindwa kusoma kwa amani kutokana na hofu waliyo nayo, jambo ambalo linawarudisha nyuma kielimu, aliomba wawasaidie kumwondoa.

Mbunge wa Jimbo hilo Aloyce Kwezi, amewataka kutafuta mtaalamu wa kukamata nyoka ili awasaidie kumwondoa kwa kuwa uwepo wake katika eneo hilo ni hatari sana na unawapa hofu kubwa walimu na wanafunzi.

‘Msitegemee maombi tu, iteni wataalamu wa kukamata nyoka waje wamwondoe, ili wanafunzi wasome kwa amani na utulivu, japokuwa sidhani kama bado yupo humo’, amesema.

Amewataka kushughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo ili maendeleo ya shule hiyo kitaaluma na miradi inayoendelea kutekelezwa isije kuathirika kutokana na hofu iliyopo, na kama watashindwa wamjulishe.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,979FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles