KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, ametamba kuwa na mwarobaini wa ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, utakaofanyika Februari 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Mayanja imekuja wakati Wekundu hao wa Msimbazi, Simba wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 2-0 toka kwa mahasimu wao kwenye mchezo wao wa mwisho uliochezwa Septemba 26 mwaka jana.
Akizungumza na MTANZANIA, Mayanja alisema kuwa yeye ni mtu wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo ndani ya timu, hivyo kipigo cha timu yake katika mchezo uliopita tayari alishapata ufumbuzi.
“Septemba mwaka jana hadi sasa ni mbali sana, ukiangalia timu yetu imebadilika vya kutosha, tayari tumeanza kupata matokeo ya ushindi hivyo sina sababu ya kuwa na presha au kupoteza muda kwa kuongea sana.
“Mashabiki wanachotakiwa ni kusubiri matokeo kwa kuwa wakati mwingi nimekuwa mtu wa kutafuta ufumbuzi wa jambo, hivyo akili yangu inafikiria kupata ushindi kuanzia mchezo wa Stand United hadi huo wa Yanga,” alisema Mayanja.
Mayanja alionesha kushangazwa na presha inayooneshwa na wapinzani wao na kudai kuwa hawapaswi kuishi kwa woga badala yake wanatakiwa kujiamini.
“Hauwezi kujizuia kutofikiria mchezo huo na hakuna sababu ya kuogopa pia kwa sasa sina haja ya kujadili sana mchezo huo kwa kuwa hautazuilika hata mara moja.
“Kwa sasa tunatakiwa kufikiria zaidi mchezo wetu dhidi ya Stand, kwa kuwa hatuwezi kufahamu endapo tutapata majeruhi au la, hivyo baada ya mchezo tutajua tuanzie wapi,” alisema Mayanja.