30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MCL, TEF walaani vikali Kazimoto kumpiga mwandishi

Mwinyi KazimotoNA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited, wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, wamesikitishwa na kitendo cha mchezaji wa timu ya Simba, Mwinyi Kazimoto kumvamia na kumjeruhi kwa kumpiga ngumi, mateke, makofi mwandishi Mwanahiba Richard anayefanya kazi katika kampuni hiyo.

Kazimoto alifanya kitendo hicho kibaya kwa Mwanahiba baada ya kumtuhumu kuwa mwandishi huyo alimuandika vibaya katikati ya mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana na Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bakari Machumu, ameeleza kuwa anaamini mwandishi alichofanya ni kutimiza wajibu wake wa kuutaarifu umma kuhusu mambo mbalimbali yanayotokea uwanjani au kwa wachezaji, hivyo Mwanahiba hana dhamira yoyote ya kumwandika vibaya mchezaji, au timu yoyote ile.

“Kazimoto kama anahisi amekosewa na mwandishi ama gazeti, jukumu lake lilikuwa ni kutaka gazeti limuombe radhi au kuchukua hatua za kisheria dhidi ya gazeti na mwandishi husika, lakini kitendo alichokifanya hakistahiki kufanywa na mtu aishiye katika jamii staarabu.

“Mchezaji huyo alishawahi kumpigia simu kadhaa mwandishi wetu, akimtusi na kumtishia kwa kumpa siku saba ili ataje mtu aliyempa habari aliyoiandika mwaka jana baada ya Simba kucharazwa bao 1-0 na Prisons ya Mbeya.

“MCL inalaani vikali kitendo hicho na tayari tunachukua hatua ya kupeleka malalamiko kwa viongozi wa Simba na tunaendelea kufuatilia hatua za kisheria,” ilisema taarifa hiyo.

 

Alieleza kuwa kitendo hicho alichofanya Kazimoto ni cha kikatili na hatukutarajia kuwa mchezaji mahiri kama yeye angeweza kufanya kitendo kibaya kama hicho, ambacho si tu kimemdhalilisha na kumuumiza mwandishi wetu, bali kimeidhalilisha kampuni yetu, waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, amekemea vikali kitendo hicho cha Kazimoto kumpiga mwandishi hadi kumjeruhi.

Akizungumza na MTANZANIA, Meena alisema kitendo hicho kinawafanya wafikirie mara mbili uhusiano wa vyombo vya habari na watu au taasisi ambazo zinakiuka uhuru wa waandishi.

“Mwandishi anapokuwa katika kazi anaongozwa na utaratibu, lakini kama binadamu wakati mwingine anaweza kukosea ni vema anapokosea achukuliwe hatua za kisheria si kumpiga.

“Hili tatizo la kuwapiga waandishi wa habari ni kubwa na limezidi kuongezeka, lilianza kufanywa na wanasiasa na sasa limehamia kwa kila mtu kutaka kuchukua sheria mkononi, hivyo ni muhimu kukemea kitendo hicho,” alisema Meena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles