26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TEMESA watakiwa kuweka fomu za mrejesho katika karakana zao

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk.Leonard Chamuriho ameuagiza Wakala wa Umeme nchini (TEMESA) kuweka fomu za mrejesho katika karakana zao ambazo zitajazwa na wateja ambao wanatengeneza magari  kuhusiana na huduma walizopewa na wakala hao.  

Hatua hiyo imekuja kufuatia Waziri huyo kudai kumekuwa na  malalamiko mengi ya baadhi ya Taasisi za umma kutoridhishwa na huduma za utengenezaji magari wanazozitoa Temesa.

Akizungumza Jumanne Mei 11, mwaka huu, Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Waziri Chamuriho amesema uwepo wa fomu hizo utasaidia kupata mrejesho wa jinsi gari lilivyotengenezwa na hivyo kuondoa malalamiko.

 “Pamoja na kuweka miundombinu wezeshi Watanzania na vitendea kazi wanatarajia kuona jitihada hizi zinaenda sambamba na kuboresha huduma za kiufundi  kwani kwa sasa yapo malalamiko mengi miongoni mwa wateja wenu hasa Taasisi za umma kutoridhishwa na huduma mnazotoa,huduma hizi kuwa chini ya kiwango ukilinganisha na hali halisi ya gharama,”amesema.

Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi, amesema kutokana na malalamiko hayo, Temesa inatakiwa kuweka mfumo wa marejesho kwa wateja ili ajaze fomu baada ya kupatiwa huduma.

“Sasa hili tutakuwa tunajitathmini, Je haya malalamiko bado yapo yanaendelea maana mmekamilika kwa kila kitu…Muweke mfumo wa mrejesho kwa wateja wenu kwa huduma zote mnazotoa kama ni gari ama kifaa chochote lazima ajeze na fomu huduma za mrejesho ili kumfuatilia.Na nyie mmelaumiwa sana sasa ni lazima mpate mrejesho,”amesema Waziri huyo.

Pia ameutaka Wakala huo kukusanya mapato katika vivuko kwa njia ya Kieletroniki ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.

“Ninafahamu mnaendelea kukusanya mapato pamoja na kudhibiti kwa kuzingatia weledi nawaagiza muendelee kufunga mifumo ya kukusanya mapato katika vivuko hivyo ili kuhakikisha mapato yote yanathibitiwa.Nawapongeza kwa kukamilisha vivuko vitatu pamoja na ukarabati wa vingine vitatu,”amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Temesa, Eng. Japhet Maselle amesema katika Mwaka wa Fedha 2020-2021, Wakala umeendendelea kutekeleza miradi mbalimbali ambayo ni ujenzi wa maegesho, ukarabati wa vivuko pamoja na miundombinu yake.

Amesema hadi kufikia Aprili 2021 Wakala umefanikiwa kununua vivuko vitatu ambavyo ni MV Kilindoni hapa kazi tu, MV Ukara 2  hapa kazi tu na MV Chato 2 hapa kazi tu.

“Pia tumefanikiwa kukamilisha ukarabati ya kivuko cha MV Sengerema na hivyo jumla vivuko kuwa 33 na boti 3, vilevile ujenzi wa maegesho na ujenzi wa vituo unaendelea pia umekamilisha ununuzi wa boti za wagonjwa tatu,”amesema.

Pia amesema wakala umeendelea na mkakati wa kuendelea kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa Kieletroniki.

Aidha, Wakala umeendelea na ukarabati wa Karakana katika mikoa mbalimbali ambapo hadi kufikia Aprili 2021 kuna  karakana 26 za mikoa na 3 ngazi ya Wilaya zimejengwa ambapo zote zimepewa vifaa.

“Hadi sasa tunawatumishi 527 wa ajira za kudumu na watumishi 485 ni wa mkataba na wahandisi ni 92 lakini mafundi sanifu 221. Pamoja na vibali hivyo tunaupungufu wa watumihsi kada ya ufundi 152 hata hivyo wakala utaendelea kuajiri watumishi wa mkataba ili kupunguza adha hiyo,”amesema

Mtendaji huyo Mkuu wa Temesa amesema Wakala unakabiliwa na changamoto za uchakavu wa miundombinu, madeni na bei ya upatikanaji wa vipuri halisi,

Amesema ili kuondokana na mzigo wanaiomba serikali kuunda mfuko wa kuhudumia magari ambao utakuwa na suluhisho katika kuhudumia magari.

“Changamoto ya upatikanaji wa vipuri halisi tumeifanyia kazi kwa kuingia makubaliano na kampuni ya Toyota na vipuri vyote vitanunuliwa kwa wingi na kwa bei nafuu na watatoa mafunzo kwa mafundi wa Temesa,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles