25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAKALA; UTOAJI MIMBA, KUHARIBIKA MIMBA NA MADHARA YAKE

Na Yohana Paul, MWANZA

SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto siku hadi siku imeendelea kufanya juhudi kubwa kupambana na vifo vya wajawazito na watoto kwa kuboresha huduma za afya hasa kwa kujenga na kuongeza idadi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Kwa kipindi cha mitano iliyopita hadi sasa serikali imefanikiwau kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99 na Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda tatu.

Mbali na juhudi hizo taarifa zinaonyesha kuwa utoaji mimba usio salama bado  kati ya changamoto kubwa ikiwa ni moja ya visababishi vikubwa vya vifo vya wajawazito kwani  unachangia zaidi ya theluthi moja ya wajawazito wanaolazwa mahospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo moja ya vifo vya uzazi.

Hadi sasa sheria na sera ya utoaji mimba nchini Tanzania ina utata na inachanganya, ambapo sheria ya makosa ya jinai inataja kosa la utoaji mimba kuwa ni jinai na huidhinisha utoaji mimba tu pale unapofanyika kuokoa maisha ya mwanamke, lakini haijaweka wazi kama utaratibu huu utalinda afya ya mwili na akili ya mwanamke.

Uwepo wa sheria hiyo imepelekea  hofu ya kushtakiwa kwa wanawake na watoa huduma ya afya wanaojihusisha na kosa hilo, na hivyo husababisha wanawake na mabinti wengi hasa walio vyuoni  watoe mimba kwa siri na kwa njia ambazo mara nyingi huwa si salama.

SABABU ZA UTOAJI MIMBA

Zipo sababu kadhaa zinozoelezea viwango vya utoaji mimba kwa wanawake  ikiwemo utofauti katika idadi ya watoto ambayo wanawake wanataka kuwa nayo, utofauti katika tendo la kujamiiana na matumizi ya uzazi wa mpango pamoja na matukio ya mimba zisizotarajiwa.

Inaelezwa kuwa takribani mwanamke mmoja kati ya watano wenye umri kati ya miaka 15–49 nchini Tanzania wanataka kuchelewesha au kusitisha kuwa na watoto lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango. Kundi hili la wanawake huchukuliwa kama lenye mahitaji yasiyofikiwa ya uzazi wa mpango. 

Kwa mfano Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa maeneo yanayoelezwa kuwa na matumizi ya chini ya uzazi wa mpango na ukubwa wa mahitaji yasiyofikiwa kiasi cha kuchangia kiwango kikubwa cha utoaji mimba na mimba zisizotarajiwa.

Aidha, imebainika, wanawake wenye mimba zisizotarajiwa kwenye maeneo mengi nchini hasa mabinti walio chini ya miaka 20 wana uwezekano zaidi wa kuamua kutoa mimba na kusababisha viwango vya juu vya utoaji mimba kutokana na kujikuta kwenye mimba zisizo tarajiwa ama mimba kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Imefahamika mimba zisizotarajiwa zimeendelea kutokana na mabinti walio wengi kuanza ngono katika umri mdogo, umri ambao wanakuwa kwenye ombwe la uelewa wa elimu sahihi ya  afya ya uzazi kwani  wanawake wanaaoanza vitendo vya ngono wakiwa na umri mkubwa, na walioolewa huripoti kiwango kidogo cha utoaji mimba.

Hapa nchini, sheria inayoruhusu kutoa mimba haipo, hivyo jambo hili ni kosa na hivyo hufanywa kwa kificho, pengine katika mazingira yasiyofaa, kukosa ujuzi wa kitaalamu na vifaa visivyo sahihi na wakati mwingine ni wasichana wenyewe hushawishiana jinsi ya kutoa mimba na kusasabisha madhara tofauti.

MADHARA YA UTOAJI MIMBA

Miongoni mwa madhara yaliyobanika kuambatana moja kwa moja na utoaji mimba ni vifo, kupoteza damu nyingi, kifafa cha uzazi na maambukizi hatarishi katika mfuko wa uzazi au mirija ya uzazi.

Pia imeelezwa kwamba madhara haya yote yanaweza kuambatana na homa kali na maumivu makali, kutunga usaha kwenye kizazi na kulazimika kufanyiwa upasuaji wa dharura au haraka kitaalamu na hata mwisho wa siku hupelekea kifo.

Wakati huo huo mhusika kama akipona kutokana na athari ya kuichokonoa mimba visivyo au kwa nguvu sana, huenda ikasababisha uharibifu wa mfuko wa uzazi na mirija yake, na kubakiwa na makovu kwenye ile ngozi laini ya mfuko wa uzazi, ambayo humsababishia maumivu makali anapokaribia siku zake za hedhi ama kuupoteza mzunguuko wake kabisa.

Wataalamu wanasema atahri hizi zinaweza kuwa ni za muda mrefu au milele ambapo kitaalamu wanaita ni kupoteza heshima ya uzazi (quality of life) huku athari nyingine zinazoweza kuambatana na utoaji mimba ni kufungwa kwa kizazi, kwani mirija ya uzazi ikijifunga basi mwanamke hawezi tena kuzaa maishani mwake.

Inaelezwa, kujifunga kwa mirija ya uzazi, husababisha mbegu ya yai la mwanaume ambayo ni ndogo kujipenyeza na kuingia, na mbegu ya yai la mwanamke ambayo ni kubwa hupita na yanapokutana kusabibisha mimba kutunga nje ya kizazi, ambayo kitaalamu huitwa “ectopic pregnancy”.

Kwa kuwa mimba hiyo iko nje ya mazingira ya kawaida, inaweza ikapasuka na kupoteza damu nyingi na kusababisha kifo na ikiwahiwa ni kufanyiwa upasuaji na kulifunga eneo hilo.

Pia utoaji mimba unaweza mfanya mhusika kupata ugumba ambao kitaalamu unajulikana kama “infertility”, hali hii inayotokana na uharibifu wa mazingira ya mpango wa mfuko wa uzazi na hasa kwa uchokonoaji wa mimba, hivyo kufungwa kwa kizazi, pengine hedhi inakoma na kwa kutopata hedhi wanawake wengi huchanganyikiwa.

Tatizo hili la ugumba huwa linasababishwa na kukwanguliwa kwa ile ngozi laini inayozunguka tumbo la uzazi, na kukwanguliwa huko kunatokana na ama vifaa vinavyotumiwa kuichokonoa mimba hiyo au madawa makali.

Athari nyingine kama uchokonoaji umepita kiasi na kufikia kwenye utumbo mkubwa huathirika na kusababisha utumbo kutobolewa na kuwekwa mrija wa kutolea choo kikubwa.

Vile vile hali hiyo husababisha ugandaji wa damu kwenye mishipa ya fahamu kuelekea kwenye ubongo, hali ambayo ni hatari mno, kwani inasababisha mhusika kuwa na hali kama ya kiharusi.

Kutokana na athari hizo na hasa ugumba, wanawake hupatwa na msongo mzito wa mawazo na kuchanganyikiwa kisaikolojia, hivyo huanza kuwa na tabia za ajabu za hasira na hata chuki kwa wenzao wenye watoto na hata kuwachukia watoto wa wenzao pasipo sababu za msingi. Wanajihisi wamekosa ule ubora wa kuitwa mwanamke.

Baadhi ya wasichana baada ya kukumbwa na tatizo la ugumba hujifariji kuwa ati wamebaki na uzuri wao na hapo hujiingiza kwenye biashara haramu ya kuuza miili yao na kujiweka kwenye hatari ya maambukizi ya magonjwa ya ngono na kupata ukimwi pia.

Ni vyema kutambua kuwa, mimba huleta ulemavu wa maisha, kutokuzaa kabisa na hata kifo, hivyo ni vyema wanawake waachane na tabia hiyo ya kuzichokonoa mimba, na waachane na kubeba mimba wasizozipanga, pia waepuke tamaa za maisha ya starehe kwani zinawatumbukiza kwenye majanga.

NINI KIFANYIKE?

Watalaamu wa afya wanashauri, ili kupunguza utoaji mimba usio salama na vifo vya wajawazito na majeraha yanayohusishwa na utoaji mimba, upo uhitaji kupanua upatikanaji wa elimu na huduma za uzazi wa mpango kuweza kuzuia mimba zisizotarajiwa, na upatikanaji wa huduma za kabla na baada ya kuharibika kwa mimba.

Aidha ni vyema vituo vya afya katika ngazi zote lazima viwe na dawa muhimu za kutosha, vifaa vya kutolea huduma za msingi za kabla na baada ya kuharibika kwa mimba, na watoa huduma wa kawaida wanapaswa wapewe mafunzo ya kutoa huduma inayohusisha afya ya uzazi.

Pia huduma baada ya kuharibika kwa mimba zitolewe sambamba na huduma za uzazi wa mpango kwa sababu wagonjwa wanaopokea huduma baada ya kuharibika kwa mimba hupokea sana ushauri nasaha juu ya uzazi wa mpango kwani tafiti zimegundua kwamba idadi kubwa ya wagonjwa hao hukubali njia za uzazi wa mpango na kuendelea kuzitumia.

Huduma baada ya kuharibika kwa mimba kutoa fursa ya kushirikisha wanaume katika uzazi wa mpango kwani iko wazi kuwa wanaume wanaokwenda na wapenzi wao kwenye huduma baada ya kuharibika kwa mimba hupokea na taarifa za uzazi wa mpango pia.

Kuondokana na utata ama changamoto za utoaji mimba usio salama, ni vyema utata kuhusu sheria ya utoaji mimba ya nchini ufafanuliwe ili kusaidia kuunga mkono taratibu salama na kisheria zitumike kikamilifu, na kuhakikisha kuwa wanawake hawana sababu ya kuamua kutumia njia za utoaji mimba zisizo salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles