NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MARUDIO ya uchaguzi visiwani Zanzibar, yamemwibua Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ambaye amepinga hatua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sheikh Ponda alisema taasisi yao haiutambui uchaguzi huo kwa sababu umeitishwa pasipo kufuata misingi ya kisheria.
“Tamko la kufuta uchaguzi lililotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha halikuwa halali kwa sababu hakuwa na mamlaka kisheria ya kufuta uchaguzi, hali inayoonyesha kwamba hadi sasa uchaguzi huo ulikuwa halali,” alisema Sheikh Ponda.
UTATA WA SHEIKH FARID
Aidha Sheikh Ponda alipinga taarifa zilizotolewa na Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alizosema kwamba Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed, ameunga mkono marudio ya uchaguzi huo wakati si kweli.
“Tumekwenda asubuhi (jana) kuonana naye Sheikh Farid na alitueleza kwamba hajaunga mkono suala la marudio ya uchaguzi bali anachokililia ni kusimamia uchaguzi wa haki,” alisema Sheikh Ponda.