Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga
Wananchi wa Mtaa wa Sokolo, Kata ya Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wameonesha kukwamisha zoezi la urasimishaji wa makazi ya mtaa huo baada ya kushindwa kuchangia gharama ya upimaji ya Sh 120,000 kwa kila kiwanja kwa muda wa miaka minne tangu kuanza kwa zoezi hilo mwaka 2017.
Akitoa taarifa ya zoezi hilo Msimamizi wa Mradi huo Afisa kutoka Ofisi ya Ardhi ya manispaa ya Sumbawanga Colman Riziki alisema kuwa wananchi hao waliafikiana katika mikutano ya mitaa kuchangia gharama hizo kwa kila kiwanja huku mtaa huo ukiwa na viwanja 911 na hivyo kutarajiwa kupatikana jumla ya Sh 109,320,000 hata hivyo wenye viwanja waliokamilisha michango yao ni 122 na waliochangia kwa viwango tofauti ni 60 na kupelekea kupatikana kwa Shilingi 17,682,000 ambayo ni sawa na asilimia 16.17%.
“Kiasi kilichochangwa cha Shilingi 17,682,000/= kimetumika chote, hata hivyo, kiasi hicho hakikuweza kutosheleza kazi zote, hivyo bado kuna madeni ya malipo ya vitendea kazi, dizeli, posho za vibarua, na wasimamizi, ingawa kazi ya upangaji na upimaji imekamilika kwa asilimia 100 huku uchangiaji ukiwa ni asilimia 16.17,” ameeleza.
Wakati akitoa nasaha zake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alisema kuwa zoezi la kupanga na kupima maeneo yaliyokuwa yameendelezwa ni suala lenye manufaa makubwa kwa wananchi na serikali kwa ujumla na kuongeza kuwa miongoni mwa faida zinazopatikana ni Pamoja na kuondoa migogoro ya mipaka, wananchi kupewa hatimiliki ambazo zinaweza kuwasaidia kukopa benki kwaajili ya kujiendeleza kibiashara, kutenga maeneo ya huduma za jamii na michezo.
“Pamojana hamasa inayoendelea kufanywa na maafisa ardhi ngazi ya halmashauri na Manispaa na Ofisi ya Kamisha wa ardhi bado zoezi la urasimishaji wa ardhi linakwenda kwa kusuasua au limekuwa na mwako mdogo wa wananchi katika kuchangia gharama ndogo zinazotozwa za shilingi 120,000 pekee kama zilivyokubaliwa katika mikutano ya serikali ya mtaa wa Sokolo,” alisema.
“Unadaiwa Sh 120,000 tangu mwaka 2017, Je, thamani ya Sh hiyo tangu mwaka 2017 hadi leo iko sawasawa? Aliyelipa wakati ule na atakayelipa leo ile thamani iko sawa kweli? Viko tofauti kwahiyo muweze kuangalia nini cha kufanya na ningefurahi sana kama mngeniambia hapa ninyi wenyewe, Je, tunapeana muda gani wa kulipa na kama watu hawakulipa tufanye nini, kama ni kupigwa faini, basi iwepo kwenye makubaliano, ili ajue umepewa mwaka mmoja kulipa Sh 120,000 na kama hukulipa basi kila unapozidi mwezi basi ulipe pengine faini asilimia moja,” alisisitiza.
Maneno hayo ameyasema katika hafla fupi ya kukabidhi hati 13 kwa wananchi wa mtaa wa Sokolo ikiwa ni uthibitisho wa kazi iliyofanya na ofisi ya ardhi katika kurasimisha makazi ya mtaa huo Pamoja na kuwaonesha wananchi kuwa hamasa iliyokuwa ikitolewa juu ya kuchangia gharama za upimaji Pamoja na kupatiwa hati kwa shilingi 120,000 ni kweli na hivyo kuwavutia waendelee kuchangia ili kazi hiyo iwe rahisi hata kwa mitaa mingine.
Wakati akitoa neno la shukran mmoja wa wananchi ambaye alipokea hati mbili katika tukio hilo ambaye pia ni katibu wa kamati ya urasimishaji ya Mtaa huo Venance Kadiba aliendelea kuwahamasisha wananchi juu ya uchangia wa gharama hizo na kuwahakikishia kuwa taratibu za kufuata hadi kuipata hati hiyo ni rahisi na gharama ni nafuu.
“Baadhi ya maneno yapo ambayo mimi niliyakuta mtaani wakati tukiendelea na taratibu hizi, mara ya kwanza kutambua viwanja kuna watu wanakuuliza hati ina rangi gani, ni vigumu kumjibu haraka lakini kwa kadiri tulivyokuwa tumewezeshwa kwa maelezo ya kujibu na nafikiri leo jibu sahihi limepatikana baada ya ninyi viongozi kufika katika eneo hili na kutukabidhi hati hizi ambazo tunaamini tumeondosha mambo mengi yanayoleta tafrani katika masuala ya ardhi,” alisema.
Mtaa wa Sokolo una ukubwa wa Ekari 550.2 na eneo lililofanyiwa urasimishaji wa makazi lina ukubwa wa ekari 137.55 sawa na 25% ya eneo lote la Mtaa wa Sokolo na pia eneo hilo ni 98% ya eneo lililojengeka ama kuendelezwa.
Urasimishaji wa Makazi katika Manispaa ya Sumbawanga unafanywa katika Mitaa Mitano ya Makutano, Sokolo, Pwela, Majumbasita, na Kasisiwe ambapo mitaa Minne ya Sokolo, Pwela, Majumbasita na Kasisiweimefanyiwa urasimishaji na wataalamu wa Manispaa ya Sumbawanga na Mtaa Mmoja wa Makutano unafanyiwa urasimishaji na Kampuni ya upimaji Ardhi ambapo jumla ya viwanja 3,314 vimeshapimwa katika mitaa yote mitano.