32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaofanya ngono umri mdogo hatarini kupata kansa

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WASICHANA wanaoanza kushiriki uhusiano wa ‘ngono’ katika umri mdogo wapo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi kuliko   wenye umri mkubwa.

Utafiti wa kitaalamu zinasisitiza kwamba hiyo ni kwa sababu kirusi cha HPV (Human Pappiloma Virus) ambacho husababisha ugonjwa huo huchukua miaka 20 kuanza kuonyesha athari  kinapoingia kwenye mwili wa mwanamke.

Hayo yalielezwa   Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Harrison Chuwa  alipozungumza na MTANZANIA kuhusu maandalizi ya Siku ya Saratani Duniani ambayo hufanyika Januari 4 kila mwaka.

“Wasichana wanaoshiriki uhusiano wa ‘ngono’ katika umri mdogo wapo hatarini zaidi kupata saratani ya shingo ya kizazi siku zijazo kuliko wale wanaoanza wakiwa na umri mkubwa.

“Utafiti unabainisha kwamba kirusi cha HPV (Human Pappiloma Virus) ambacho husababisha ugonjwa huu huchukua miaka 20 kuanza kuonyesha athari kwenye miili yao,” alisema.

Alisema   pia umeweza kubainika ukweli wa jambo hilo kutokana na idadi kubwa ya wanawake wanaosumbuliwa na tatizo hilo wanaokwenda kupata matibabu kuwa  na umri wa miaka 45.

“Huwa tunapokea takriban wagonjwa 22,000 kwa mwaka wanaofika kutibiwa kwenye taasisi yetu kwa saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ambao ni  asilimia 40 ya wagonjwa wote.

“Tumebaini kwamba wanawake wanaougua saratani hii ni wale walioko kwenye umri wa miaka 45. Tukitazama na utafiti, tunakadiria kwamba huenda walianza kushiriki uhusiano huo wakiwa na umri wa miaka 25 kushuka chini,” alisema.

Alisema wasichana wanaoshiriki uhusiano huo na wanaume wengi huwa katika hatari zaidi kuliko wale wanaoshiriki na mmoja.

Alisema matatizo ya saratani yanazidi kuongezeka na idadi ya wanaofika  hospitalini inaongezeka.  “Hii tunajua ni kwa sababu ya jamii kupatiwa elimu kwamba magonjwa hayo yanatibiwa,” alisema na kuongeza:

“Tunajua tatizo hili kwa kiasi fulani linachangiwa na umasikini… wakati mwingine wapo wanaojihusisha  waweze kujikimu katika maisha.

“Hata hivyo ni vema wasichana wakajitunza na kuacha kufanya matendo hayo wakiwa katika umri mdogo   kujiepusha na uwezekano wa kupata saratani hii siku za usoni.”

Alisema saratani nyingine zinazoongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa katika taasisi hiyo ni za matiti, koo la chakula, kichwa na shingo.

“Kwa upande wa saratani ya tezi dume yenyewe inashika namba 11   hapa hospitalini, pengine ni kwa sababu wanaume hawajitokezi wengi kupima afya zao kuliko ilivyo kwa wanaume,” alisema.

Alisema vipo vyanzo mbalimbali vinavyochangia mtu kupata saratani ambavyo ni uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na unywaji wa pombe.

“Kwa ujumla ni kwamba mfumo wetu wa maisha wa siku hizi unachangia kupata maradhi haya, watu siku hizi hatufanyi mazoezi na tunapenda zaidi vyakula vya kufungashwa kuliko vile vya asili,” alisema

Alisema taasisi hiyo imeandaa utaratibu wa kupima afya bure  kuchunguza saratani mbalimbali siku ya maadhimisho hayo ambayo   mwaka huu yamepewa kaulimbiu inayosema:

‘Tunaweza, Ninaweza…sote kwa pamoja na kila mmoja ana jukumu la kukabiliana na athari au janga la saratani’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles