29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa: Bunge lipinge utawala wa mabavu

Dr-Slaa-4Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa ameibuka na kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

Dk. Slaa ambaye kwa sasa yuko   Canada, amesema kutokana na hali ya mambo yanayoendelea hivi sasa nchini ni jukumu la Bunge kuhakikisha utawala wa mabavu unaofanywa na baadhi ya viongozi   madarakani hautokei.

Akizungumza na MTANZANIA  mwanzoni mwa wiki  akiwa   Canada, Dk. Slaa, alipongeza uongozi wa Rais Dk. John Magufuli akisema   yale aliyokuwa akiyapigia kelele kwa zaidi ya miaka 10 sasa yanatekelezwa.

“Kwa siku 100 ambazo Rais Magufuli yuko ofisini nadhani kama kuna jambo ninatakiwa kusema ni kumpongeza, kumtakia heri.

“Huko nyuma nilitoa kauli kwenye mtandao kuwa jukumu sasa ni la Bunge, bila itikadi ya vyama, kumsaidia Rais hayo aliyoyaanza yaweze kutekelezwa, kuhakikisha kuwa framework (utaratibu) sahihi wa kulinda haki kwa maana marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu   inapohitajika.

“Pia ni jukumu la Bunge kuhakikisha udikteta unaohofiwa na baadhi ya watu hautokei.  Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘ukiachiwa atakuwa dikteta’.  Vyombo vyote vifanye kazi kwa mujibu wa Sheria,”alisema Dk. Slaa.

Alipoulizwa kuhusu hatima yake katika siasa, alisema tangu alipoondoka Oktoba mwaka jana kwenda  Canada  ambako anasoma mambo mbalimbali alisema;

“Kabla ya kuondoka Tanzania niliwaaga Watanzania kwa programu kadhaa zilizorushwa live (moja kwa moja). Niliwaaga kuwa naenda ‘sabbatical’,  kwa lugha nyingine nitasoma mambo mbalimbali.

“….nilishawahi kueleza kuwa kwa sasa ninasoma Psychoanalysis na Psychotherapy (kwa kuzingatia kuwa Major Seminary nilisoma idara zake zote ikiwa ni pamoja na Psychology). Hivyo bado nasoma ninanoa akili zangu,” alisema Dk. Slaa.

Akizungumzia   kuuzwa kwa nyumba yake iliyopo Mbweni  Dar es Salaam  baada ya kushindwa kurejesha mkopo wa benki, alisema yeye na mke wake hawajawahi kuchukua mkopo wa aina yoyote benki.

“Nataka nikuambie na uwajulishe Watanzania kwamba wala si mimi Dk. Slaa wala mke wangu, Josephine kwa wakati wowote ule hatujawahi kuchukua mkopo benki.

“Tangu nimetoka bungeni sijawahi kuchukua hata senti moja benki, achilia mbali propaganda ya Sh milioni 300.

“Hivyo ni vizuri waliokupa taarifa wakupe undani ni benki ipi nilikopa au Josephine alikopa na ni shilingi ngapi na kwa nyaraka zipi tulikopa. Ni vema pia ukafuatilia na benki husika kama walikuambia ni benki gani.

“Na sisi huku tunasikia taarifa ya nyumba yetu kuuzwa. Kwa hatua ya sasa sidhani kuwa ni suala la kwenye magazeti. Ninachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria dhidi ya wote waliohusika,” alisema.

MTANZANIA ilipotaka kujua maoni yake kuhusu hali ya siasa Visiwani Zanzibar hasa baada ya kufutwa matokeo Oktoba 28, mwaka jana na kutangazwa uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu, alisema kwa vile kipindi chote amekuwa nje ya nchi hivyo hawezi kuzungumzia kuhusu suala hilo.

“Mambo ya Zanzibar yana sura ya sheria na procedure (utaratibu) ikiwa ni pamoja na taratibu zilizotumika. Kipindi chote hicho nimekuwa nje.

“Sina tabia ya kukurupikia jambo ambalo sina taarifa kamili nalo. Taarifa pekee zinazopatikana ni za kwenye mitandao ambayo wewe mwenyewe ni shahidi kuwa mengi yanawekwa chumvi au hata kutengenezwa kwa sababu za propaganda.

“Mimi niko nje ya ‘active party politics’ kama nilivyotangaza Septemba Mosi mwaka jana, hivyo siendekezi propaganda wala mambo yaliyowekwa chumvi au hata yale ambayo siyafahamu vizuri,” alisema Dk. Slaa.

Katibu Mkuu huyo wa zamani ya Chadema, alitangaza kujiengua katika uongozi Septemba Mosi  mwaka jana baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujiunga na chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles