NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema ugonjwa wa kipindupindu umepungua kwa asilimia 12 nchini huku ikisisitiza bado kuna changamoto kutokana na mikoa mingine kuendelea kuongoza kwa ugonjwa huo.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John, ilisema ugonjwa huo umepungua kwa kiasi kikubwa huku Mkoa wa Simiyu ukiwa katika hali tete.
“Zipo changamoto kadhaa ambazo zinatukabili kukabiliana na ugonjwa huu ikiwamo ya idadi ya kaya ndogo kutumia vyoo bora, hususan maeneo ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa huu ukiwamo Mkoa wa Simiyu,” alisema John.
Alisema kutokuwapo miundombinu stahiki kama vile vyoo na maji katika maeneo ya mikusanyiko kama masoko na minada, kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
Taarifa hiyo ilisema jopo la wataalamu litakwenda mikoa ya Morogoro, Dodoma, Simiyu, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Mwanza na Mara kuhamasisha utumiaji wa kanuni za afya.
Kutokana na hali hiyo, John ameziagiza mamlaka za mikoa na halmashauri na watendaji wake kote nchini kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa mlipuko huo.
Wakati huohuo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhamed Bakari, ametoa tahadhari kwa wananchi kujikinga na ugonjwa mpya wa homa ya Zika ambao unasababishwa na kirusi kijulikanacho kama Zika.
Alisema ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi takriban sita za Afrika ambazo ni Afrika ya Kati, Misri, Gabon, Sierra Leone, Tanzania na Uganda.
“Pia ugonjwa huu upo katika nchi za India, Indonesia, Malaysia, Philippines, Thailand na Vietnam na pia nchi za Amerika na Pacific na hadi sasa umeathiri watu wengi Amerika ya Kusini.
Alisema ugonjwa huu unaenezwa na mbu wa Aedes, ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana na jioni. Aina hiyo ya kirusi ipo katika
familia ya “flavirus” ambako pia wapo virusi vya ugonjwa wa dengue, homa ya manjano (Yellow fever), Japanese ancephalitis na West Nile Virus.