Na Renatha Kapaka, Bukoba
DIWANI wa Kata ya Kimwani Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Silvester Miga (55) wa Chama cha Wananchi (CUF), amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini, baada ya kuvamiwa na kukatwakatwa mapanga nyumbani kwake.
Tukio la kuuawa kwa diwani huyo lilitokea usiku wa kuamkia jana, akiwa nyumbani kwake akiangalia taarifa ya habari katika runinga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alisema Miga alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kagondo wilayani Muleba.
Ollomi alisema tukio hilo lilitokea wakati diwani huyo akiangalia runinga nyumbani kwake.
“Wahalifu walivamia na kufanya mauaji haya kwa kumshambuliwa Miga kwa mapanga na kutoweka kusikojulikana.
“Baada ya hali hiyo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Kagondo kwa matibabu lakini kutokana na kujeruhiwa vibaya na kutokwa na damu nyingi alifariki dunia majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Ullomi.
Alisema Jeshi la Polisi lilifanya msako na kuwatia mbaroni watu wawili ambao wanadaiwa kuhusika na tukio hilo.
Kamanda aliwataja waliokamatwa kuwa ni Aderarid Antony (42) na Shiranga Gonzari (22) ambao jeshi hilo linaendelea kuwahoji.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Muleba wamesema kuuawa kwa diwani huyo kuna mazingira ya siasa.
Wananchi hao walilitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili waliofanya mauaji hayo wabainike na kufikishwa katika vyombo vya sheria.