29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NEC: Magufuli hana mamlaka ya kuingilia

MagufuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI Watanzania wakiwa na shauku ya kusikia Rais Dk. John Magufuli anatoa kauli juu ya hatima ya mtanziko wa siasa Zanzibar, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema hana mamlaka ya katiba kuingilia suala hilo.

Kauli hiyo ya NEC imetolewa huku tayari kiongozi huyo wa nchi akiwa amekutana na mahasimu wa siasa Visiwani humo, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye anawania nafasi hiyo kupitia CCM pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Kutokana na mtanziko huo, jana Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva,  alisema Rais Dk. Magufuli hana mamlaka  ya katiba kuingilia uamuzi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Jaji Lubuva alitoa kauli Ikulu  Dar es Salaam baada ya kuwa na mazungumzo na Rais Dk. Magufuli.

“Rais hana mamlaka katika katiba pia ya kuingilia uamuzi NEC kwa upande wa Tanzania Bara,” alisema Jaji Lubuva.

Katika mazungumzo hayo, Jaji Lubuva alimpa taarifa Rais Magufuli juu ya mambo yaliyojiri katika kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika  Kampala ambacho kilijadili   Uchaguzi Mkuu wa Uganda, unaotarajiwa kufanyika Februari 18, mwaka huu.

Jaji Lubuva alisema wanaosema Rais anapaswa kuingilia  masuala ya uchaguzi iwe Tanzania Bara au Zanzibar, wanafanya makosa kwa sababu  kwa namna yoyote hana mamlaka hayo.

“Unaposikia  Rais wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama kujikanganya huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa halafu unasema aingilie kati uamuzi ya tume.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika katiba hana mamlaka ya kuingilia uamuzi wa ZEC wala NEC,” alisema.

Jaji Lubuva, alimhakikishia Rais Magufuli kuwa tume hiyo ipo huru na kwamba haijawahi kuingiliwa katika uamuzi na rais, wala uongozi yeyote.

Kuhusu kikao kilichofanyika Uganda ambacho yeye alikuwa mwenyekiti, alisema kilihusu umuhimu wa tume ya uchaguzi kuwa huru.

Alisema kikao hicho kilichukulia mfano wa Tanzania ambayo imetoka katika uchaguzi mkuu miezi michache iliyopita.

UCHAGUZI KUFUTWA

Oktoba 28  mwaka jana, ZEC ilifuta matokeo yote ya uchaguzi mkuu, baada ya kubainika kujitokeza kwa kasoro nyingi zilizosababisha kukiukwa   sheria za uchaguzi na haki kushindwa kutendeka.

Mwenyekiti Jecha Salim Jecha, alisema ZEC imefanya utafiti na kujiridhisha na hatimaye kuamua kufuta matokeo yote ya uchaguzi ili urudiwe.

Alisema hakuna mgogoro wa katiba  unaozuia mchakato huo kuendelea na imewataka Watanzania kupuuza upotoshaji wa tafsiri ya sheria, unaofanywa na baadhi ya watu na kueleza kuwa mchakato utaendelea kama kawaida.

Pamoja na kuwapo na hali hiyo, Maalim Seif alijitangaza mshindi kinyume cha sheria na taratibu za uchaguzi ambazo zinaipa ZEC uamuzi wa kutangaza matokeo hayo.

 

TAMKO LA MABALOZI

Januari 29 mwaka huu mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) walieleza kusikitishwa na kitendo cha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio Visiwani humo,  wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro yakiendelea.

Walimtaka Rais Dk. John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua sintofahamu ya  siasa Zanzibar.

Taarifa yao ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mabalozi hao jana, pia inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka pande zote zitafute suluhu kwa amani.

Tamko hilo limetolewa siku chache baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza  uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani utarudiwa Machi 20  mwaka huu, ikiwa ni siku chache tangu CUF kutoa azimio la kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza Kuu.

Mabalozi hao wamelaani kitendo hicho wakisema kurudia uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiuka, kinawatia wasiwasi kwa kuwa tume hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.

Mabalozi hao walisema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU, Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC, Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.

“Tunasikitika kuwa ZEC imetangaza tena kuwa uchaguzi utarudiwa Zanzibar, wakati mazungumzo baina ya pande mbili yanaendelea.

“Kwa manufaa ya Watanzania wote, tunasisitiza kuwa hali ya siasa ya Zanzibar ni bora ikatatuliwa kwa pande mbili kukubaliana,”  ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilitumwa kwa ushirikiano wa Mabalozi wa Uholanzi, Norway, Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden, Uswisi, Uingereza, Ireland na Marekani.

Inasisitiza kuwa kitendo cha upande mmoja kuamua kurudia uchaguzi  kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni mwa Wazanzibari.

“Tunawaomba Wazanzibari kuwa watulivu na wavumilivu nyakati hizi na tunazitaka pande zote mbili na washirika wao kuendelea kufanya kazi pamoja ili wapate suluhisho la amani,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema ili uchaguzi uwe wa kuaminika, mchakato wake hauna budi kuziwakilisha pande zote na kuwa huru na wa haki.

Mabalozi hao wamesema kulingana na mazingira ya Zanzibar kwa sasa, itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa kutegemewa kushiriki kwa namna yoyote katika uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles