33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ebola yatikisa Kenya

Shirika la Afya Duniani
Shirika la Afya Duniani

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limetahadharisha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki uko katika kundi la pili lenye uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa wa Ebola, kutokana na ukaribu wake na maeneo yaliyoathirika na mlipuko wa ugonjwa huo unaoenea kwa kasi.

Hali hiyo inatokana na Kenya kuwa kitovu cha usafiri wa ndege, huku wasafiri wengi wanaokwenda nchi za Afrika Magharibi wakipitia nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, WHO imetoa onyo kali kuhusu kuenea kwa ugonjwa huo katika eneo la Afrika Mashariki.

Wataalamu wa afya wanasema wanafanya jitihada kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo Afrika Magharibi, ambako zaidi ya watu 1,000 wamefariki dunia.

Mkurugenzi wa WHO nchini Kenya, Custodia Mandlhate, ametoa onyo hilo juzi huku hatua za kuzuia maambukizi na kutambua wagonjwa zikishika kasi katika mataifa yote ya Afrika Mashariki.

Waziri wa Afya wa Kenya, James Macharia, alisema pamoja na hatari hiyo, nchi hiyo haitasitisha safari zake kwa nchi nne za Afrika Magharibi.

“Hatushauri safari za ndege kusitishwa kwa sababu ya mipaka yetu ambayo watu wanaingia na kutoka pasipo vikwazo vingi,” alisema Macharia.

Kenya ina zaidi ya safari 70 za ndege kutoka Afrika Magharibi kila wiki.

Pamoja na tamko hilo la Serikali ya Kenya, WHO imeitaka kuimarisha juhudi za kukagua, kugundua na kukabiliana na virusi vya ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa WHO nchini Kenya, Dk. Mandlhate, alisema hali hiyo inachangiwa na ukweli kwamba nchi hiyo haiko mbali na maeneo ambayo yameshuhudia mlipuko wa Ebola.

“Katika ramani tunaweza kuiorodhesha Kenya katika kundi la pili ambalo limo katika hatari kubwa ya kuambukizwa,” alisema Dk. Mandlhate.

Alisema hatari zaidi ya kuenea kwa Ebola kutoka mataifa ya Afrika Magharibi, inatokana na ukweli kwamba ugonjwa huo huenea kwa kasi.

“Hii ni kwa kuzingatia kuwa maambukizi hutokea pia katika vituo vya matibabu. Pia, maeneo yaliyoathirika hayana mfumo thabiti wa afya.

“Serikali inapaswa kujiweka tayari. Inapaswa kuwa na juhudi kamilifu kukabiliana na hali hii na kuhusisha wadau wote ikiwemo sekta binafsi, jamii na sekta ya umma.

“Kama tulivyoona, asilimia 55 ya waathirika waliaga dunia,” alisema Dk. Mandlhate.

Alisema mlipuko unaweza kutokea baada ya siku 42 baada ya kisa cha kwanza kuthibitishwa.

“Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha ugonjwa huo unachunguzwa, kugunduliwa na hatua zifaazo kuchukuliwa kuzuia kuenea.

“Ebola inazidi kuenea na huenda baadhi ya taarifa hazijabainika katika vituo vya afya. Hatuwezi kujua hali hii itaendelea hadi lini hadi baada ya siku 42 baada ya kuthibitishwa.

“Hivyo ni muhimu kwa Kenya kujiweka tayari kuzuia kuingia na kusambazwa kwa ugonjwa huo na kwingineko,” alisema Dk. Mandlhate.

Hata hivyo, alisifu Serikali kwa juhudi zake za kuhakikisha ugonjwa huo haufiki nchini humo kupitia hatua kabambe zilizochukuliwa, na kuahidi WHO itaendelea kuisaidia katika juhudi hizo.

Shirika hilo tayari limetangaza Ebola kama changamoto ya afya ya kimataifa.

Canada imesema itatoa mchango wa dozi 1,000 za chanjo ya majaribio ya Ebola kusaidia watu kutoambukizwa.

Taarifa ya kwanza ya Ebola iliripotiwa nchini Guinea Februari mwaka huu kabla ya kuenea hadi nchini Sierra Leone na Liberia.

Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika, na hivi karibuni iliripotiwa kuwa na theluthi moja ya vifo kutokana na Ebola.

Jumuiya ya Uchumi Afrika Magharibi (ECOWAS), imesema mmoja wa maofisa wake, Jatto Asihu Abdulqudir, mwenye umri wa miaka 36, alifariki dunia kutokana na Ebola.

Hadi Agosti 11, mwaka huu watu 1,013 wamefariki dunia na huku taarifa za watu 1,848 wanadaiwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo.

Ndege zasitisha safari

Shirika la ndege la Kenya Airways hata hivyo lilisema ni nadra kwa ugonjwa huo kuambukizwa kupitia kwa abiria kwa sababu watu hawana mgusano wa moja kwa moja.

Liliongeza kuwa huenda kufungwa kwa mipaka kati ya mataifa kusisaidie kuzuia maambukizi kwa sababu huenda baadhi ya taarifa zinaweza kutotambuliwa hasa katika maeneo ya mipakani.

Juzi, shirika hilo liliahidi kutoa taarifa leo kuhusu hatima ya safari zake za ndege Afrika Magharibi huku kukiwa na taarifa kwamba Shirika la Ndege la Korea limetangaza kusitisha safari zake nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles