27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Mawaziri wakwamisha Bunge la Katiba

Bunge
Bunge

Esther Mbussi na Fredy Azzah, Dodoma

WAKATI vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vikiendelea mjini Dodoma, uamuzi wa kamati umeshindwa kuafikiwa, MTANZANIA limebaini.

Kutokana na hali hiyo, idadi kubwa ya wajumbe kutoka Tanzania bara wengi wao wakiwa mawaziri, hawahudhurii vikao vya kamati vinavyoendelea.

Mbali na wajumbe hao, imebainika pia zaidi ya wajumbe 80 ambao hawatoki kwenye kundi linalounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawajaripoti kwenye Bunge hilo tangu lilipoanza shughuli zake Agosti 5, mwaka huu.

Baadhi ya wenyeviti wa kamati wameliambia MTANZANIA kuwa hivi sasa uamuzi umekuwa ukikwama kupita kutokana na kukosekana kwa akidi.

Wenyeviti hao walisema licha ya utoro, kuchelewa kufika kwa wajumbe kunachelewesha kuanza kwa vikao hivyo, na kanuni za Bunge Maalumu la Katiba  zinawataka wasifanye chochote kama theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande zote za Muungano haijatimia.

Wakati mawaziri hao na wajumbe kutoka Bara wakidaiwa kuwa na mahudhurio hafifu na utoro, wajumbe kutoka Zanzibar wamekuwa wakiwahi na kuhudhuria vikao hivyo vya kamati bila kuwapo dharura.

MTANZANIA lilimtafuta Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, ambaye alikiri kuwapo kwa hali hiyo ya utoro, na kusema kuwa ana imani Bunge zima litakaporejea kwa ajili ya kupiga kura hali hiyo itaisha.

Alisema kuwa ripoti wanazopata kutoka kwa wenyeviti wa kamati mbalimbali zinaeleza kuwa uchelewaji ni tatizo kubwa.

“Wanatuambia kuwa uchelewaji ndio tatizo, tumewaambia wasianze vikao bila akidi kutimia kwa sababu watu humo humo ndani watakuja kusema kuwa akidi ilikuwa haitimii kwenye vikao.

“Kwahiyo wakati mwingine wanalazimika hadi kuwapigia watu simu na kuwasubiri, lakini tumewashauri wasianze vikao hadi akidi itakapotimia na itakapofika wakati wa kupiga kura kwa Bunge zima, itabidi wote waje sasa,” alisema.

Katibu huyo alisema kuwa hadi sasa wajumbe wa Bunge hilo waliofika Dodoma ni 432 pekee kati ya 629.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe 83 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kundi la 201 ndio ambao hawajaripoti hadi sasa.

Alisema wajumbe wa Ukawa kwa kuangalia vyama vyenye wabunge vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, ni 115.

Pamoja na hali hiyo, alisema kuwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar na Bara itapatikana hata kama Ukawa hawatarejea kwenye Bunge hilo.

“Theluthi mbili inayotakiwa ni 420 kwa sababu Bunge lote lina watu 630, kwa hawa wajumbe wote ambao wako kwenye vikao vya kamati sasa hivi kama watapiga kura, theluthi mbili itapatikana kwa pande zote.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati Namba 12, zinaeleza wajumbe kutoka Zanzibar ndio pekee wanaowahi katika vikao hivyo bila kuwa na dharura wala kuchelewa kama ilivyo kwa baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania Bara.

Mmoja wa wajumbe kutoka kamati hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema theluthi mbili kutoka Zanzibar imekuwa ikipatikana kwa wakati kuliko kutoka Bara.

Alisema wajumbe wengi ni watoro na kwamba kutokuwapo kwa Ukawa hakujabadilisha kitu katika majadiliano yanayoendelea kwa upande wa theluthi mbili kutoka Zanzibar na mvutano wa kutokukubaliana katika kupitisha na kurekebisha baadhi ya vifungu ni mkali.

“Bara ndiyo inasumbua kwa sababu ya viongozi, hasa mawaziri walikuwa nje, pia kuna wabunge hawapo, unakuta Mzanzibari kaingia kama mfugaji.

“Tunachojaribu kuangalia, kile tunachokijadili kinajadiliwa kwa kina, kama hadi leo kuna kamati nyingine hazijamaliza sura mbili kutokana na mvutano wa kutokubaliana kutokuwa mwepesi kama watu wanavyodhani kwamba Ukawa hawapo basi mambo yatapita tu,” alisema.

Alisema wajumbe wa CCM wenyewe hawakubaliani kwenye baadhi ya mambo, kuna wengine wanapinga na wengine wanakubaliana mambo yanayotakiwa, kwahiyo na wenyewe pia hawako pamoja.

“Pia tukumbuke katika kundi la 201 ni watu ambao wengi hawafungamani na upande wowote, hawakubaliani na mambo kwa sababu sisi tunaona huko nje, tunajua watu wanachokihitaji, kwahiyo si rahisi kupitisha kirahisi.

Kuhusu mgawanyo wa madaraka ambapo kwa sasa mawaziri wanatokana na ubunge, alisema suala hilo ni tete kutokana na wenye kofia hizo kulitetea, lakini walio wengi hawakubali kwa hoja.

Alisema hatua hiyo imekuwa ikipingwa na wananchi kwa muda mrefu, ambapo mtu mmoja anakuwa na kofia kadhaa za uongozi, ikiwemo kuwa waziri, mbunge, mjumbe wa bodi, mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles