26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI WA VURUGU

 

 

  • Wafuasi, mgombea udiwani wapigana visu Arusha
  • Lema apigwa mateke, polisi waingilia kati
  • CCM, Chadema watoshana nguvu Buyungu

ELIYA MBONEA Na NORA DAMIAN, ARUSHA/DAR


UCHAGUZI mdogo wa ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma pamoja na udiwani kata 36, umefanyika huku mgombea na wafuasi wakipigana visu mkoani Arusha.

Uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Kaloleni Jimbo la Arusha Mjini, uliingia dosari baada ya kuibuka vuruga kutokana na baadhi ya watu kuchomwa visu.

Pamoja na vurugu hizo gari la mgombea udiwani wa Kata ya Daraja Mbili, Masud Sungwa (Chadema), linadaiwa kuchomolewa tairi la nyuma na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM, huku watu waliokuwa ndani ya gari hilo walilazimika kushuka na kukimbia ili kunusuru maisha yao.

Vurugu zilitokea jana Kata ya Kaloleni ambapo msaidizi wa mgombea udiwani kupitia Chadema, Ibrahimu Mussa anadaiwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye jicho la kushoto, huku mgombea wake Boniface Kimaro akikabwa shingo.

Katika vurugu hizo Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kaloleni, lddi Mussa alidai kuchomwa kisu begani na kujeruhiwa maeneo ya mwili wake na mmoja wa aliyekuwa kwenye kundi la wafuasi wa Chadema waliokuwa wamemzingira.

Vyanzo vya habari kutoka eneo la tukio vilidai vurugu hizo zinadaiwa kusababishwa na baadhi ya vijana na wafuasi wa CCM walioanza kumshambulia kwa mateke mgombea wa Chadema Kimaro.

Akizungumzia tukio hilo jana mjini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi alisema mgombea wa Chadema alishambuliwa na watu wasiojulikana.

“Amekwisha kufungua kesi tayari kituo cha polisi kwa ajili ya kuanza uchunguzi. Aliyechomwa kisu ni mwanachama wa CCM alikuwa eneo la Mianzini jiji hapa.

“Huyu alikutana na kundi jingine na kulitokea mzozo baina yao ndipo mmoja wapo kwenye kundi hilo alimchoma kisu mfuasi wa CCM.  Mtu huyo tunamshikilia kwa mahojiano,” alisema Kamanda Ng’anzi.

Alisema kwa ujumla uchaguzi mkoani humo unaendelea vizuri kwa kata tatu za Jimbo la Arusha ukiachilia mbali Kata ya Kaloleni kulikoibuka mzozo kidogo ambao tayari umeshaanza kufanyiwa kazi na jeshi hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, akielezea kuhusu kilichotokea alisema, alipata taarifa za vurugu hizo na kisha kutoa taarifa ya kuomba askari kwa RPC Ng’anzi.

“Mimi baada ya kufika pale eneo la tukio mmoja wa wafuasi wa CCM alinitemea kohozi kisha nikaanza kushambuliwa kwa mitama na kupigwa katikati ya bunduki za polisi, kiongozi wa polisi aliyekuwa pale akaniambia gari la polisi jingine linakuja.

“Lilipofika bado wale wafuasi wa CCM hawakukamatwa, tulikwenda polisi kwa ajili ya kupewa PF3 ili akimbizwe hospitalini kwa matibabu.

“Taifa hili linakwenda kubaya kupita kiasi, mtu amechomwa kisu bado waliohusika wamemfuata mpaka hospitali. Ulishaona wapi ujasiri wa mtu kuchomwa kisu anaumizwa anajitetea lakini bado anakamatwa yeye na anapewa kesi.

“Mgombea wetu wa udiwani yupo hospitali bado alifuatwa na kutaka kuendelea kupigwa mbele ya polisi. Tumeshauriana na Katibu Mkuu wa Chama Taifa pamoja na Meya wetu wa Jiji la Arusha Calist Lazaro.

“Tayari Katibu Mkuu wa chama ametupa maelekezo teundelee na uchaguzi mpaka mwisho, kwetu sisi tulikuwa tumekuja hapa kwa ajili ya kuwaambia madiwani wetu wajiondoe, lakini kwa vile wametuambia tuendelee tutaendelea.

“….huyu Idd anayedai amechomwa kisu kimsingi yeye ndio alikuwa anamchoma visu kwa taarifa ambazo nilizipata pale kwenye eneo la tukio, na polisi wanao mkanda mzima wa tukio lote lililotokea,” alisema Lema.

Alisema Kata ya Daraja Mbili, vijana wa CCM walivamia gari la mgombea wetu wakatoboa tairi la nyuma kwa Sime, wakashusha waliokuwamo ndani kisha wao kukaa kwenye gari wakaanza kunywa pombe.

“Hii ni dharau ya hali ya juu sana tumebakiza saa chache sana kumalizia uchaguzi huu ombi letu wananchi waendelee kujitokeza kupiga kura.

“Kwa maana hii ni matumaini yangu kwa Kamati Kuu ya Chama iamue tunatumia mbinu gani nyingine kutetea Watanzania kwani mbinu ya kura katika taifa hili haiwezekani tena,” alisema

Naye Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya  Doita (Chadema), akifafanua kuhusu tukio hilo alisema lilitokea saa 4 asubuhi wakati mgombea huyo akiwa kwenye kituo cha kupigia kura Kaloleni.

“Mgombea alikuwa ameongozana na wafuasi wake kwenda kupiga kura ghafla lilitokeza kundi la wafuasi wa CCM wakaanza kumshambulia kwa kumpiga mateke mwilini na hapo ndipo msaidizi wake alichomwa visu.

“Nimeshuhudia kwa macho yangu jinsi wafuasi wa Chadema walivyokuwa wakishambuliwa mbele ya askari Polisi na hakuna mtu yeyote aliyehusika aliyekamatwa. Msaidizi wa mgombea Ibrahimu amechomwa visu jichoni, tumboni, miguuni na maeneo mengine ya mwili,”alidai Doita.

Alisema kundi hilo la vijana huenda limepewa kazi maalumu na viongozi waliopewa dhamana kutokana na kutokamatwa pindi walipofanya uhalifu huo.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kaloleni, Idd Mussa aliyedai kuchomwa kisu na wafuasi wa Chadema alisema akiwa maeneo ya Tanki la Maji Kaloleni alikutana na kundi la wafuasi wa Chadema walioanza kumshambulia.

“Nilikuwa nimesimama mahali waliponikaribia wakaanza kunirushia mawe nami nikaokota kwa lengo wa kuwarushia kwa lengo la kujihami.

“Ghafla walinizunguka na kuniweka kati, mmoja kati yao alikuwa amenishikilia ndipo nikajikuta nimechomwa kisu begani,” alisema Mussa.

Wakati huo huo mgombea wa Kata ya Usunyani Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chadema, Joseph Albert alipinga taarifa zilizosambazwa kuwa amejitoa kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha na Diwani wa Kata ya Kikatiti,  Jimbo la Arumeru Mashariki , Elisa Mungure, alisema hawakujitoa kwenye uchaguzi Kata ya Songoro.

“Kilichotokea mgombea wetu alikamatwa na polisi asubuhi akanyimwa dhamana na mimi ndio nikawa nimeenda kumuwekea dhamana kituo cha polisi.

“Lakini pia wakala wetu mkuu ambaye ni Diwani Penzila Pallangyo, alipigwa vibao viwili na wakala wa CCM tumemepela Hospitali ya Usa River kwa matibabu kwani haoni vizuri.

“Achilia mbali hao wapo mawakala wengine wamezuiliwa kuingia kwenye vituo vyao, kimsingi tulikuwa tunakwenda vizuri lakini baadaye kukawa kumeharibiwa,” alisema Mungure.

Akifafanua baadhi ya tuhuma hizo Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alidai wafuasi wa Chadema ndio walionza kumshambulia kiongozi wa CCM Kata ya Kaloleni.

“Taarifa za vurugu hizo zilipomfikia Mbunge Lema alikwenda moja kwa moja kwenye tukio na akiwa pale alimshambulia kwa kichwa mfuasi mwingine.

“Nimshukuru Katibu wangu wa CCM Mkoa kwani aliliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha lisimkamate Lema badala yake wamwache aendelee na uchaguzi ili isionekane CCM inatimia vibaya vyombo vya dola.

“CCM haina lengo baya, sisi tunataka kuendeleza amani na kulinda utulivu uliopo kama Chama kinachoongoza Serikali,” alisema Mdoe.

KAULI YA DAKTARI

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Dk. Elias Mashalla alithibitisha kupokelewa kwa wagonjwa hao wawili akisema walikuwa katika hali nzuri na waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu.

Alimtaja majeruhi Kimaro alikuwa na majeraha machache mwilini na alipofanyiwa vipimo vya X Ray walibaini kuwa hakuwa amevunjika eneo lolote la mwili wake zaidi ya kuwa na kidonda kidogo mdomoni, alipatiwa dawa na kuruhusiwa.

“Majeruhi mwingine ni Mussa aliyekuwa na mpasuko mdogo kwenye jicho lake kwa juu ambalo halikutokana na kisu kwani jeraha la kisu lisingeweza kuwa dogo na asingeruhusiwa kurudi nyumbani.

“Jicho lake linaona vizuri ni sehemu ya juu ndio palipasuka tumemshona na anaendelea vizuri, “ alisema Dk. Mashalla.

Uchaguzi huo mdogo kwa Mkoa wa Arusha ulikuwa na Kata 20 zilizokuwa zinashirki uchaguzi ambapo kati ya Kata hizo 13 CCM ilipita bila kupingwa na hivyo kata 7 ndizo zilizoshiriki uchaguzi huo wa marudio.

CUF WALALAMA

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Mneke Jafar, alisema baadhi ya mawakala wao walizuiwa kuingia vituoni katika Kata za Lyoma mkoani Mwanza na Peramiho mkoani Ruvuma.

“Baadhi ya maeneo wasimamizi wanahujumu uchaguzi, mawakala wetu walizuiwa kuingia vituoni na mpaka inafika saa 3 asubuhi walikuwa hawajaruhusiwa. Katika Kata ya Lyoma yenye vituo 15 mawakala wetu walizuiwa katika sita,” alisema Jafar.

Mkurugenzi huyo alidai kuwa dosari katika uchaguzi huo zilianza tangu wakati wa kampeni na kwamba katika baadhi ya maeneo CCM kinatumia nguvu ya ziada kwa kufanya figisu mbalimbali ili kushinda.

“Wanazunguka na magari kujaribu kuwatisha wananchi, tunaliomba jeshi la polisi lisitumike kukisaidia CCM,” alisema.

Alisema wamesimamisha wagombea katika kata 14 na Jimbo la Buyungu na wamejipanga kuibuka na ushindi mzuri hasa katika kata wanazozitetea ambazo ni Navingu, Makonga, Makorola, Magwekweni, Kabila na Lyoma.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles