NA BENJAMIN MASESE
MGOMBEA ubunge Serengeti kwa tiketi ya CCM, Dk. Steven Kebwe amesema anafurahia kuona Ukawa ukishindwa kuelewana na chama kinachosimamisha mgombea Serengeti.
Amesema hadi sasa vyama hivyo vipo katika mvutano mkubwa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha NCCR Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), kitendo ambacho kimesababisha kuwapo makundi.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu kuhusu siku anayotarajia kuzindua kampeni jimboni humo, Dk. Kebwe alisema jinsi hali ilivyo ndani ya Ukawa, inaonyesha wazi tayari wameshindwa mapema kabla ya uchaguzi.
Dk. Kebwe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alidai wananchi waliokuwa na imani na Ukawa jimboni humo, tayari wamekata tamaa na kujiunga na CCM kitendo ambacho kimemfurahisha na kumpa urahisi wa kampeni hadi siku ya uchaguzi.
“Hivi tunavyozungumza na wewe natoka jimboni nakwenda Dar es Salaam kukamilisha baadhi ya mambo ya Serikali Septemba mosi nianze kampeni, ninachokiona jimboni kwangu ni kusubiri kuapishwa kwa sababu hadi sasa Ukawa hawajui wafanye nini.
“Kila chama kinataka kusimamisha mgombea wake, sasa hali hiyo imewafanya baadhi ya wananchi waliokuwa na imani nao kujiondoa na kuja kwangu. Mimi ni chaguo la wananchi kwani itakumbukwa hata wagombea wa CCM waliokuwa wamechukua fomu walijiondoa baada ya kuona nakubalika sana.
“Ndani ya miaka mitano nimebadilisha jimbo kwa kuboresha sekta ya afya, elimu na miundombinu, leo ukifika hospitalini unakuta madaktari wanakusubiri tofauti na ilivyokuwa awali, zahanati zimeongezeka na nyingine zimepandishwa hadhi.
“Hakuna sekta ambayo sikuifanyia kazi, nimejenga majosho, malambo, maabara, barabara zimetengenezwa huku vijana wameanza kunufaika na Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti, sasa miradi ambayo haijamilika nitakamilisha kwa kipindi kijacho, naomba wananchi kuwa na imani na mimi,” alisema.