NA OSCAR ASSENGA, TANGA
KAYA 40 zenye watu zaidi ya 100 zimelazimika kuhama makazi yao na kuhifadhiwa kwa muda katika Shule ya Msingi Magaoni kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafurikiko jijini Tanga.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, baadhi ya waathirika hao wameitupia lawama Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kushindwa kuchimba mfereji wa kusafirishia maji ya mvua jambo linalochangia kutokea kwa mafuriko katika makazi yao.
Fatuma Hamisi alisema walishatoa taarifa kwa uongozi wa Jiji la Tanga kuhusu hali hiyo, lakini suala hilo limekuwa likipuuzwa na hata kusababisha madhara kwao.
“Baadhi ya waathirika wa mvua hizo ambao wengi wao ni kinamama na watoto wamekwenda kuhifadhiwa katika chumba cha darasa na baadhi yao wakilazimika kuhamisha vyombo vyao katika maeneo mengine,” alisema Fatuma.
Kutokana na mvua hizo, ilikilazimu Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufanya kazi ya uokoaji ambapo kiliwaokoa watoto watatu waliokwama katika moja ya nyumba za eneo hilo kwa kuzidiwa na maji.
Kiongozi wa kikosi hicho aliyekuwa akiongoza timu ya waokoaji, Koplo Halfani Mhina, alisema watoto hao walikuwa wamesahaulika ndani ya chumba huku maji yakiwa yamejaa hali iliyowalamu kuvunja milango.