22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mwandosya, Makongoro leo, Kamani, Ngeleja kesho

mwandosyaNA WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI

UTANGAZAJI nia ya kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeanza kwa kishindo, huku machifu wote wa Mkoa wa Mbeya wakitarajiwa kumuunga mkono Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, ambaye leo anatarajiwa kutangaza nia mkoani Mbeya.

Miongoni mwao ni Chifu wa Rungwe, Mbozi na Chifu wa Jiji la Mbeya, Mwashiga ambaye atawaongoza pia wazee wote wa jiji hilo.

Wakati hayo yakijiri, wakazi wa Jiji la Mbeya wakiwamo vijana, pia wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza Profesa Mwandosya kutangaza nia.

Hafla hiyo inayotarajiwa kufanyika saa nne asubuhi, itafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo eneo la Soko Matola jijini Mbeya.

Katika hafla hiyo, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyo nje ya Ukawa wanatarajiwa kuhudhuria ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kutoa msimamo wao wa kumuunga mkono Profesa Mwandosya.

Vyama hivyo ni TLP, ACT-Wazalendo, APPT- Maendeleo,  UDP, PP, SAU na UPDP.

Wakati Mwandosya akiwa Mbeya, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere naye anatarajia kutangaza nia ya kuwania urais kijijini kwao Mwitongo wilayani Butiama.

 

NGELEJA, KAMANI KESHO

Wakati hayo yakijiri, Mbunge wa Sengerema mkoani Mwanza, William Ngeleja pamoja na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani wao wakitarajiwa kutangaza kesho jijini Mwanza.

 

NYALANDU NA FOMU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema siku saba zijazo kuanzia sasa atachukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais wa Tanzania.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha baada ya kumalizika ibada ya kwanza aliyoshiriki katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha mjini.

“Nimekuja kanisani kuabudu, nimefarijika kwa neno la Mungu. Nataka kusema, nilishatangaza nia miezi saba iliyopita, Desemba mwaka jana,” alisema Waziri Nyalandu na kuongeza:

“Nia haitangazwi mara mbili na siku saba baada ya miezi saba kuanzia sasa hivi nitachukua fomu, historia itaandikwa upya ya nchi yetu, amani iwe nanyi,” alisema Waziri Nyalandu.

 

MEMBE JUNI 6

Kwa upande waje Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema atatangaza nia ya kuwania urais Juni 6, mwaka huu jimboni kwake Mtama mkoani Lindi.

Kutokana na utangazaji nia unaoendelea sasa, amewataka Watanzania kuwapima na kuwachunguza viongozi wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Akizungumza jana wakati wa tamasha la kaswida lililoandaliwa na Taasisi ya Ulamaa Promotion Centre, Membe alisema ni muda mwafaka sasa wa kuwapima wagombea na matendo yao.

 

Habari hii imeandaliwa na Eliya Mbonea, Christina Guluhanga na Veronica Romwald (Dar), Fredrick Katulanda (Mwanza), Pendo Fundisha na Sarah Mossi, (Mbeya).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles