30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Tembo wazidi kuteketea

TemboELIAS MSUYA NA AZIZA MASOUD

WAKATI nusu ya tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wakidaiwa kupukutika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kutokana na ujangili, Serikali ya Tanzania inadaiwa kukalia ripoti ya kupungua kwa tembo nchini.
Taarifa ya kupungua kwa nusu ya tembo katika hifadhi hiyo imetolewa katika sensa ya wanyama hao iliyofanyika kwa miaka miwili kwa kupita juu ya mbuga za wanyama na kuangalia mgawanyiko wa tembo kwa Afrika nzima.
Sensa hiyo ilifadhiliwa na mwanzilishi wa Taasisi ya Microsoft, Paul Allen katika mradi wake mkubwa wa kuhesabu tembo ulioanza mwaka 1970.
Serikali inadaiwa kupokea ripoti hiyo Januari mwaka huu lakini hadi sasa imeshindwa kuitoa hadharani kwa kile inachodaiwa kuwa inataka kwanza kufanya uchunguzi zaidi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu hakuwa tayari kuzungumzia ripoti hiyo wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau wa maendeleo na asasi za kiraia zilizopo nchini uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Nyalandu alikiri kuwa ujangili wa tembo bado ni tatizo na ripoti ya sensa ya mwaka jana iliyomfikia inaonyesha kuwa, katika Mbuga ya Wanyama ya Selous, idadi ya wanyama hao ilikuwa 13,084 wakati 2009 walikuwa 38,975.
Ujangili Hifadhi ya Ruaha
Katika ripoti hiyo iliyoonyeshwa na Kituo cha Televisheni cha ITV News cha Uingereza, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inaelezwa kupoteza nusu ya tembo wake kutoka 8,500 waliokuwepo mwaka 2014 hadi 4,200 waliopo sasa.
Watafiti wanasema katika eneo hilo lenye mbuga za wanyama na vitalu vya uwindaji, ujangili ni wa kutisha na kwamba idadi imepingua kutoka 20,000 waliokuwapo mwaka 2013 hadi 8,200 waliobaki sasa.
“Uwiano wa tembo madume wenye umri zaidi ya miaka 40 waliokuwa wakithaminishwa kwa wingi wa meno yao sasa idadi yao imeshuka kwa asilimia 72,” inasomeka taarifa hiyo.
Inaeleza zaidi kuwa ujangili unaoendelea katika hifadhi hiyo hauna tofauti na unaotokea katika Pori la Akiba la Selous, ambapo asilimia 67 ya tembo waliuawa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Katika mkutano wa jana, Waziri Nyalandu alisema upungufu wa tembo unaashiria hatari ya kutoweka kwa wanyama hao katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Waziri Nyalandu alisema mtandao wa uhalifu ni mkubwa na upo kila mahali, hivyo kuna haja ya kufungua mipaka kwenda katika maeneo mengine ambayo watakuwa na ulinzi zaidi.
Misitu
Kuhusu uvunaji holela wa misitu, Waziri Nyalandu alisema misitu inapotea kwa kasi nchini kutokana na kuwapo kwa wimbi kubwa la ukataji na uchomaji misitu.
Alisema Tanzania ina hekari 47,1000 (milioni 47) za misitu na kati ya hizo 3,50,000 zinapotea kila mwaka kwa kukatwa na kuchomwa moto.
“Matumizi ya nishati ya mkaa yanaathiri misitu, Jiji la Dar es Salaam linapokea asilimia 10 ya mkaa unaokatwa, Tanzania ikiendelea hivyo itakuwa jangwa baada ya miaka kadhaa,” alisema Nyalandu.
Alisema Serikali inamiliki asilimia 35 pekee ya misitu wakati asilimia 65 inamilikiwa na Serikali za Mitaa, vijiji na taasisi binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles