29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SIANGA JAHAZI LIPO MIKONONI MWAKO

Paul Makonda akiteta jambo na Rogers Sianga

NA INNOCENT NGANYAGWA,

KAMA kuna wakati ‘Tafakuri Yangu’ ilitatizika ni wakati huu wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hasa staili ya awali ya kuwataja hadharani washukiwa kisha kutakiwa kuripoti polisi kwa mahojiano.

Baadhi ya majina hayo walikuwamo  wanasiasa, viongozi wa dini, wasanii na wafanyabiashara. Majina ya watu maarufu yaliteka hisia za Watanzania na kuibua mijadala mizito katika vijiwe mbalimbali.

Kama ilivyo hulka ya Watanzania wengi ni kuimba wimbo wa ngoma bila kutambua mashiko ya dhamira ya mtunzi. Kwa sasa hamkani imetulia kwa kuwa si suala la utamu wa ngoma kuingia kucheza bali ni mpigaji mwenye matao ameingia ngomani na mikong’osio imekuwa sadifu.

Kama kuna wakati imani juu ya uendeshaji vita dhidi ya mihadarati imetuingia basi ni wakati huu huku tukiamini ushindi utapatikana, hususani weledi unapotamalaki baada ya kukabidhiwa kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Waliomwangalia kwa wajihi na kutilia shaka namna atakavyosimamia jukumu lake ni wazi amedhihirisha kuwa upele umepata mkunaji.

Alichotamka katika hotuba yake katika hafla ya kumkaribisha iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na kinara wa mapambano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na waathirika wa dawa hizo, alidhihirisha kuwa Rais hakukosea kumpa nafasi hiyo.

Sianga amefafanua mengi ambayo mwanzoni hayakuwekwa wazi, zaidi ya hamkani za kutajana majina na mhemko wa utashi wa kisiasa uliosaidia kwa sehemu kubwa kufanikisha kadhia ya dawa za kulevya kuongelewa hadharani bila hofu na ujasiri wa kujitokeza ‘wapambanaji’ katika sekta mbalimbali.

Sianga amebainisha mengi katika mpangilio unaoeleweka: Matumizi, athari, mbinu za wasambazaji, mbinu za kukabiliana nao na uzingatiaji wa sheria katika kukabiliana na dawa za kulevya.

Kama mapambano haya yangeanza kwa kuzingatia sheria mpya ya kupambana na dawa za kulevya iliyoundwa mwaka juzi, ingesaidia sana kuepusha hamkani zisizokuwa na maana. Kwa kiasi fulani zilitugawa, walikuwapo wanaounga mkono kutajwa majina na kushikiliwa rumande kwa washukiwa ili kubaini uhakika wa kuhusika kwao, upande wa pili kwa waliopinga njia hiyo ambayo imewawezesha wahusika wengine kujiandaa kukwepa kukabiliwa na mkono wa sheria kwa kuendesha biashara hiyo haramu.

Kuna wakati hata vyombo vyetu vya usalama hususani Jeshi la Polisi vilikuwa njiapanda, vikitimiza wajibu huku vikipingwa na waliotaka kuzingatiwa kwa sheria katika kutekelezwa mapambano hayo.

‘Tafakuri Yangu’ iling’amua kukosekana kwa utayari na mikakati sadifu ya kuendesha vita hii kwa kukasimu utekelezaji baada ya utashi wa kisiasa kuchukua nafasi yake bila kuwaachia weledi kutekeleza wajibu wao.

Sehemu kubwa ya Watanzania wanaunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya lakini si kwa namna ilivyokuwa ikiendeshwa, kwa kuwa si vita ya muda mfupi, hata mataifa makubwa hayajaweza kuimaliza zaidi ya kupunguza athari licha ya kupambana nayo kwa miaka mingi.

Kama biashara yenyewe haramu inazalisha ‘tija chafu’ ya kifedha na wanaoiendesha wanajilimbikizia mbinu na mikakati kwa kutumia fedha zao chafu, basi katika kupambana nayo inahitajika mikakati endelevu yenye ubora zaidi ya mbinu za wasambazaji na wauzaji.

Kwa kuwa tunavuka madaraja ya kadhia hiyo kutoka kuwa wapitishaji hadi kuwa waagizaji na watumiaji, tulipo sasa ni wasambazaji hivyo tusipodhibiti madaraja mawili yatakayofuata tutakuwa wazalishaji kutokana na ghafi zitakazoingizwa lakini hatua kubwa zaidi ni kuwa wazalishaji wa ghafi hitajika.

Kimsingi hatua za kuzima biashara hii zimekuja katika wakati mwafaka ili tusipande madaraja ya mihadarati bali kujitakasa, kwa hiyo kwa ‘Tafakuri Yangu’ inavyoona ni kwamba sasa ni wakati wa kuwaachia weledi watimize kazi yao, kama watakuwa wamejipanga kutokana na alivyotuaminisha Kamishna Sianga kwa ushirikiano na vyombo vyetu vya usalama, hakika tunakwenda kushinda vita hii. Ikiwa tutaigubika hamkani za kisiasa hakika tunakwenda kushindwa vita hii kwa kuwa kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa.

Kama tutajipanga na kuwekeza vya kutosha katika mapambano haya kwa kuimarisha mbinu, mafunzo, vifaa na utaalamu wa tunaowategemea katika kuongoza mapambano, basi tutazuia athari na kubadilisha mwelekeo ili kujipapatua kutoka katika janga hili baya.

Wakati huu wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya tumkumbuke Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye utawala wake ulianzisha mchakato wa upitishwaji wa sheria ya kupambana na dawa za kulevya. Alipata kusema kuwa kama tunajenga nyumba moja hatutakiwi kugombea fito na tukihausha kauli yake hiyo: ‘Kama tunapambana na adui mmoja (dawa za kulevya) hatupaswi kupambana wenyewe kwa wenyewe bali tuelekeze nguvu zetu dhidi ya madhalimu wanaotuharibia Taifa letu huku wakijineemesha.

Mungu yuko upande wetu, hakika tutashinda!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles