27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

VITA YA USHOGA TOFAUTI NA DAWA ZA KULEVYA

NA JIMMY CHARLES,

NAPINGA na kuchukia vitendo vya ushoga na usagaji. Matendo haya ni haramu, hayakubaliki duniani na mbinguni.

Matendo haya yalimchukiza Mungu miaka dahari nyuma, kwa hasira aliuteketeza Mji wa Sodoma ambao unatajwa kuwa mji uliokuwa kati ya Palestina na Yordan za leo.

Mji huu unatajwa kuwa kielelezo cha dhambi duniani na sifa yake kuu ni ushoga uliomghadhabisha Mungu ambaye aliamua kuuangamiza kama vitabu vya dini vinavyoeleza.

Ghadhabu hiyo ya Mungu inayoelezwa kwenye maandiko ya dini, inafungua ufahamu wa ubaya wa matendo ya kishoga na usagaji.

Ni kweli si jambo lenye kupendeza machoni hata kidogo na linapaswa kupingwa na kila mtu, hata hivyo naamini wapo baadhi ya wanasiasa wanataka kulitumia jambo hili kwa manufaa yao kisiasa badala ya kusaka suluhu ya kweli ya jambo hili, ambalo ni kubwa kuliko inavyodhaniwa.

Ajabu ni pale baadhi ya wanasiasa waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, kulifanyia mzaha suala hili na kutaka kulitumia kwa nia ya kusaka umaarufu.

Inasikitisha kuona kiongozi anakosa mbinu na mikakati thabiti ya kukabiliana na tatizo hili, badala yake anataka kukanyaga nyayo za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye kwa sasa anatajwa kuwa mmoja wa viongozi wachache maarufu nchini.

Kiongozi bila kufikiria anatangaza kuwa na orodha ya majina ya mashoga, hatua iliyokuja siku chache baada ya Makonda kutaja orodha ya washukiwa wa utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Nikiri wazi kuwa uamuzi wa kutaka kupambana na ushoga si mbaya, lakini si kwa mtindo huu wa kuiga. Hautasaidia kulitatua tatizo, badala yake linaweza kuamsha ari ya ‘mabasha’ kutaka kuwapitia hao waliotajwa.

Ipo haja ya muhusika aliye na utayari wa kupambana na tatizo hili la ushoga kutofautisha namna ya kupambana na jambo hili.

Makonda ingawa amekosolewa, lakini ameweza kushughulika na watu wa dawa za kulevya kwa sababu ni rahisi kumjua teja, lakini pia mkuu wa mkoa amelishughulikia jambo hili ndani ya eneo lake dogo la mkoa, tofauti na waziri au naibu waziri ambao watalazimika kulishughulikia jambo hili kwa mtazamo wa nchi nzima.

Nafasi ya waziri au naibu waziri haishii kwenye wilaya au mkoa mmoja, inagusa nchi nzima. Wigo huu wa kiutendaji wa waziri au naibu ndio unaoleta ukakasi wa kushughulika na vita hii kwa sababu watu wanajiuliza mapambano haya yatafanyika Dar es Salaam pekee kwa kuwataja akina Kaoge au yatagusa maeneo yote ya nchi na je, unawezaje kujiridhisha kuwa huyu ni shoga au huyu siye.

Suala la ushoga ni tofauti kabisa na la dawa za kulevya. Si rahisi kuuthibitisha ushoga wa mtu kwa kumwangalia, mavazi au kujipodoa kwa mtu hakumpi sifa mbaya ya ushoga kwani wapo wanaume wenye heshima zao, lakini wanashiriki mapenzi ya jinsia moja.

Viongozi wanaoongozwa na mikurupuko wanapaswa kutambua kuwa mashoga ni ndugu, jamaa, watoto na rafiki zetu na wanaofanyia hivyo ni jamii hiyo hiyo.

Kundi hili limezaliwa katika familia ambazo bila shaka hazijihusishi na shughuli hii, jambo ambalo linalazimisha kujiuliza kuwa ni wapi jamii ilipokosea na kuamua kujiweka mbali na watu hawa ambao leo hii tunawaona ni wahalifu na wakosaji wakubwa.

Jamii inastahili lawama hizi, kwa sababu hatuwasaidii kuondoka hapo walipo na tunashiriki kikamilifu kuwafanya wawe hivyo walivyo leo kwa kujua ama kutokujua.

Kama nilivyoeleza mwanzo, suala hili la ushoga limeanza karne nyingi, halijaanza jana wala leo kama lililivyovaliwa njuga kwa wanasiasa kubeba silaha nyepesi za kuwataja mashoga huku mabasha wakiachwa.

Waliopewa dhamana wanashindwa kusaka njia sahihi za kupambana na hatari hii kwa kutoa elimu na kueleza ukweli, badala yake zinatumika njia za kulikuza jambo hili kwa kushughulika na watu waliokwishaharibika.

Hakuna anayethubutu kujadili na vijana  kuhusu suala hilo mpaka leo hii, mambo yanaonekana kuwazidi nguvu na kuibuka na hatua zao za zimamoto zinazolenga kuwaadhibu hata wasiohusika.

Ukweli ni kwamba hakuna kiongozi anayetaka kujishughulisha na chanzo cha tatizo, badala yake wanakurupuka kwa namna za kuahirisha tatizo kisha kutumia mwanya huo kujipatia kura za kurejea madarakani.

Leo utatangaza orodha ya mashoga na pengine utahitaji waripoti polisi, baada ya hapo nini kinafuata je, utakuwa umewasaidia hao mashoga uliowakamata au utakuwa umepeleka chakula cha mabasha mahabusu?

Hivi kuwataja hadharani ni njia ya kulikomesha tatizo hilo au nia ni nini hasa?

Nashauri, ni vema viongozi wakapima kauli zao kabla ya kuzitoa hadharani, lakini pia kama kiongozi anayo dhamira ya dhati ya kutaka kupambana na tatizo, anapaswa kusaka njia sahihi za kulitokomeza tatizo hata kama itamchukua miaka 100.

Si vema kusaka njia za mkato katika kupambana na mambo yanayoliumiza Taifa, matokeo yake ni kudhalilisha watu na kuliacha tatizo likitamalaki.

Mungu Ibariki Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles