30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 31, 2023

Contact us: [email protected]

TAMAA YA VYEO ITAWAANGAMIZA WANYONGE

Baadhi ya mahakimu na wafanyakazi wa Idara ya Mahakama Zanzibar.

Na Balinagwe Mwambungu,

WANACHAMA wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wenye matumaini ya kuteuliwa na kushika nafasi za juu katika mahakama na vyeo vingine katika taasisi za kimahakama, bora wajitoe katika chama hicho.

Imeelezwa kuwa makada na wakereketwa wa vyama vya siasa, wasitegemee kuteuliwa na mamlaka teuzi (ya sasa) kuwa majaji.

Ndivyo baadhi yetu tulivyolipokea tamko la Rais John Magufuli, alipokuwa anazungumza na wanasheria wakati wa Siku ya Sheria iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwezi huu.

Tunaweza kwenda mbele zaidi, kwamba watu wote wenye taaluma zao, wahandisi, madaktari, walimu pamoja na waandishi wa habari na wengineo wenye matumaini na matarajio ya kuteuliwa kwenye ngazi yoyote ya juu, hawatakiwi kuwa wakosoaji, wakereketwa, wanaharakati au wanachama wa chama cha upinzani.

Taasisi ya Rais na zinazoongozwa na wateule wake ambazo zina madaraka ya kirais (by proxy) ya kumfanya nani awe na nani na nani asiwe kwenye ngazi fulani ya juu.

Tukiangalia taaluma ya sheria, tunatishika kwa sababu kama kweli kuna wanasheria wenye mawazo hayo, wataacha kusimamia haki ya kuwatetea watu wanaopelekwa mbele ya Pilato na kuacha misingi na miiko ya taaluma yao, kwa sababu tu wanaongozwa na tamaa ya kupata vyeo. Kwa msingi huo taifa letu litakuwa la wanyanyasaji, wasiginaji wa sheria na taifa lenye watu katili na wenye kuonea wanyonge. Watendewa ambao ndio wengi, watakuwa kama kondoo ambaye mmiliki akitaka kumchinja amle nyama hunyamaa. Inafikirisha!

Kwa upande mwingine, tunawatazama waandishi wa habari ambao kazi yao kubwa si tu kutangaza habari, bali pia kuwapa sauti wasio na sauti.

Kwa taswira tunayoiona kama nilivyoeleza hapo juu ni kwamba, waandishi wakifuata mwenendo huo, wataacha kuwa wapashaji habari, watageuka kuwa kasuku wa kurejea wanavyosema watu wenye mamlaka.

Itabidi waandishi waachane na miiko ya uandishi ambayo pamoja na mambo mengine, inawataka kutopendelea upande mmoja, kuwapa sauti wanyonge na wenye kutuhumiwa kwa jambo lolote.

Waandishi wa habari watakapoacha kufukua mambo mabaya ambayo walio madarakani hawataki yajulikane, basi tutakuwa tunawakilisha tuliyoyabeba kama ‘conveyor belt’, mpira unaendeshwa kwa mashine na kubeba mzigo ghafi kutoka mgodini hasa madini. Vyombo vyote vya habari vitaimba wimbo mmoja tu wa watukufu wa mamlaka. Tutakapofika hapo sijui itakuwaje. Sipati picha!

Kwa upande mwingine, jamii yetu ndivyo ilivyo. Kuna watu katika nyanja zote za kitaaluma, wanaofikiri kutokosoa wanayoyafanya watawala ni sifa moja ya kufikiriwa katika uteuzi wa kushika vyeo vya juu serikalini na katika taasisi zake.

Watu kama hao wamejaa unafiki, wazandiki, uzabizabina na wachonganishi. Wanajikomba kwa wakubwa. Katika taaluma ya habari na taaluma nyinginezo, hata katika taasisi za kidini, watu kama hao hawakosekani.

Tulijionea wazi wazi wakati wa kampeni mwaka 2015 jinsi waandishi walivyokuwa wamegawanyika, kila mwandishi alikuwa na mgombea wake, hasa kwenye kiti cha urais. Vyumba vyetu vya habari viligeuka kuwa uwanja wa siasa.

Nakumbuka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, gazeti moja lilijinasibu pasi na shaka kwamba lilikuwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Likaenda mbali zaidi likakubali kuvikwa jalada la kijani lenye maneno: Chagua CCM.

Wakuu wetu, labda kwa kumfurahisha mwenye mali, ambaye ni mwanachama mwandamizi wa chama au kwa matumaini kwamba mgombea wa urais, angewakumbuka katika teuzi wa nafasi mbalimbali. Kwa bahati mbaya, si wote waliobahatika. Wengi wao walikata tamaa baada ya kutoteuliwa hadi mtu wao anamaliza kipindi chake cha urais.

Kwa hiyo, Rais Magufuli anajua kwamba wanasheria na wanataaluma wengine, wanategemea kwamba wakati ukifika, wanaweza kufikiriwa na kuteuliwa kushika nafasi za juu kama ujaji.

Na waandishi hasa walio katika ngazi ya uhariri, wanaona kilele cha uandishi ni kuwa Mwandishi wa Rais au Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu. Kama si kwenda Ikulu, basi ukuu wa mkoa au wilaya.

Ukiwa katika nafasi ya uhariri, unaweza kuandika kwamba Rais amekosea katika jambo fulani. Ukiwa Ikulu au mteule wa Rais kwa nafasi yoyote ile, huwezi kumweleza Rais kwamba hukubaliani na jambo fulani. Utakuwa hujipendi.

Enzi zile za chama kimoja, wahariri na waandishi hawakuwa na uchaguzi, ambaye alikuwa si mwanachama wa CCM, hakuteuliwa kushika nafasi ya mhariri mkuu. Lakini hata wakati ule wanachama tulijulikana kwa makundi ya makada, wenye mlengo wa kati, wahafidhina na wenye msimamo mkali, lakini wote waumini wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Hata baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi, waandishi wengi na wahariri, wameendelea kuwa ‘affiliated to’, kuwa sehemu ya CCM. Wachache walikihama chama hicho na kujiunga na vyama vingine.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wengine walitupa karata zao kuutafuta uongozi wa kisiasa kupitia CCM na wengine kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa matumaini yale yale, kupata uteuzi endapo mgombea wao angeingia Ikulu.

Wengine waliojiunga na Ukawa si kwa sababu kutafuta uteuzi, bali walijiunga na kundi kubwa la Watanzania lililokuwa linataka mabadiliko. Aliyekuwa mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli, ndiye Rais wa Tanzania. Kuna kundi kubwa si la wahariri na waandishi tu ambalo bado lina matumaini kwamba huenda mamlaka teule ikawaona kipindi cha pili au pindi nafasi zinapotokea kuwa wazi.

Nimezungumzia zaidi taaluma ya habari kwa vile niko humo, ninajua. Taaluma inakaribiana na taaluma ya sheria, kwa sababu waandishi wanatakiwa kujua sheria kwa kiwango fulani, hasa zile zinazohusiana na taaluma ya habari na zile ambazo moja kwa moja zinahusu haki za binadamu.

Lililotisha zaidi ni kauli ya Rais Magufuli kwamba mawakili watakaosimama kuwatetea wahalifu waliokamatwa wakitenda makosa, majangili wanaojulikana, wakamatwe na kuswekwa rumande. Wako wanaosema Rais Magufuli hakumaanisha aliyosema, bali ilikuwa ni utani! Hii ilikuwa ni Siku ya Sheria, Rais ndiye kipekee anayejua kama alikuwa anatania au la.

Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, aliposema akichaguliwa ataua mapapa wa dawa za kulevya, walifikiria alikuwa anatania. Taarifa za Shirika la Al Jazeera lenye makao makuu Doha, Quarter, limeripoti hivi karibuni kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya iliyoanzishwa na Rais Duterte, imegharimu maisha ya watu takribani 6,000.

Kama Rais wetu alikuwa anatania, basi ulikuwa ni utani mbaya. Katiba yetu inatamka kwamba mtu hahesabiwi kuwa ana kosa hadi pale mahakama itakapothibitisha. Ndiyo maana watu hata wakijua kwamba wametenda kosa, wanapelekwa mahakamani. Mahakama inatazama si ushahidi dhidi ya mtuhumiwa, pia inaangalia mazingira yaliyomfanya mtuhumiwa atende kosa husika.

Nawasilisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles