27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

2017: DUNIA BADO INAKABILIWA NA MIGOGORO SUGU

kansela-angela-merkel-wa-ujerumaniZIMESHATIMIA siku nne tangu mwaka mpya uanze ingawa kwa muktadha wa kalenda inayotumika zaidi duniani, kama ambavyo hatusherehekei mwaka kwa pamoja kutokana na muda kutofautiana kutokana na eneo husika, lakini pia mustakabali wa dunia umegubikwa na migogoro endelevu iliyovuka mwaka.

Kwamba wanaoishi katika maeneo yenye migogoro mwaka mpya ni mabadiliko tu ya tarakimu, lakini hawana matumaini kimaisha kutokana na kumaliza mwaka kwenye mizozo na kuuanza mwingine katika hali hiyo.

Tukumbuke baadhi ya figisu zilizovuka mwaka zinazotarajiwa kuendelea kwenye baadhi ya maeneo yasiyotarajiwa kuwa na mabadiliko. Tuanzie nchini Marekani ambako hakuna vita lakini ujio wa utawala mpya wa Rais Mteule Donald Trump mnamo majuma mawili na ushei yajayo, lazima utabadilisha mzani wa jinsi dunia inavyoshughulikia migogoro mbalimbali.

Trump anayeonekana kama ‘Timu B’ ya ‘Timu A’ ya Rais Vladimir Puttin wa Urusi, tayari ameshatoa kauli nyingi tata baada ya kushinda uchaguzi, ikiwemo kutotilia maanani Jimbo la Krimea lililomegwa na Urusi kutoka nchi ya Ukraine, ukiwemo msimamo wake ulioipa nguvu Urusi kuivurumisha Aleppo katika mapigano yanayoendelea nchini Syria.

Ambapo usemi wa fahari wawili hawakai zizi moja umedhihirika kwa Serikali ijayo ya Marekani kuinyamazia Urusi kumeiwezesha kushirikiana na Rais Assad, kuwavurumisha waasi hadi kuwalegeza kiasi cha kukubali mwafaka wa usitishaji mapigano.

Tayari mji huo unaandaliwa kwa urejeo wa wakazi waliokimbia. Majaribio ya awali ya kusaka suluhu chini ya usimamizi wa Marekani na Urusi yalishindikana mara kadhaa, lakini Urusi ambayo kwa Marekani ni kama Mungu wa Kirumi aitwaye Janus aliyesababisha jina la mwezi wa kwanza wa mwaka (Januari) mwenye sura mbili ‘uhasimu na urafiki’ japo wa mashaka, imetafuna fupa lililoishinda Marekani kuligegedua.

Lakini pia ikituhumiwa kudukua mitandao ya Marekani na kusababisha anguko la Hillary Clinton kwenye uchaguzi, ili kuzuia muhula wa tatu wa Obama kupitia kivuli cha mgombea huyo wa Democratic aliyegaragazwa na Trump kwa msaada wa timu ya kampeni ya Trump yenye watendaji wengi wenye mwelemeo wa Urusi.

Chama cha Republican hakipendezwi na ‘uswahiba’ wa Trump na Puttin na hatua ya Obama kuwatimua wanadiplomasia wa Urusi, inamweka kikaangoni Rais Trump kwani Rais wa Marekani analazimika kuzingatia ushauri wa CIA kuhusu usalama wa taifa.

Ni suala la kusubiri kama Trump atamgeuka Puttin au atageuka kunguru mlafi atakayetaka kuhudhuria hafla mbili kwa wakati mmoja na kuishia kuchanika msamba! Ulaya nako hamkani si shwari kutokana na uamuzi wa Uingereza kujiondoa katika jumuiya ya Ulaya uliojipatia jina maarufu la ‘BREXIT’ hatua inayoashiria mwendelezo wa athari.

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Ufaransa Aprili 23, mwaka huu mgombea wa chama cha National Front mwanamama Marie Lepen, atakayechuana vikali na Francois Fillon wa Republican, ameahidi kuwa akishinda ataitisha kura ya maoni kuhusu kusalia ama kujiondoa EU kama ilivyofanya Uingereza inayoshabikiwa nchini humo, kiasi cha kupewa mtaa wenye jina la Brexit katika mji wa Beaucaire.

Ikiwa Marie atafanikiwa inamaanisha kuwa umoja huo ambao ni mshirika muhimu wa maendeleo barani Afrika unaanza kumong’onyoka taratibu, katika wakati ambao Ulaya inapaswa kusimama pamoja kukabiliana na changamoto nyingi zikiwemo ilizojipakulia makaa mdomoni kutokana na kuingilia uendeshaji wa mataifa mengine kwa ushawishi wa Marekani.

Ulaya inalipa gharama kubwa za wimbi la wahamiaji haramu wanaotishia kugharimu madaraka ya baadhi ya viongozi, mmojawapo ambaye amekalia kuti kavu ni Kansela wa Ujerumani, Angela Markel, anayekabiliwa na uchaguzi mnamo siku 39 kutoka sasa.

Salama ya muungano wa Markel wa CDU/CSU ni kumuunga mkono mgombea wa chama cha Social Democratic Party, Frank Walter Steinmeier, kwa kuwa akipata viti vingi katika Bunge (Bundestag) atamhakikishia Kansela Merkel kurudi upya madarakani kwa kuwa nafasi hiyo huchaguliwa na Bunge na haipigiwi kura na wananchi ambao humchagua Rais.

Ukiachana na Ulaya na changamoto zake lakini Mashariki ya Kati na bara Asia bado kunafukuta kwa kuwa licha ya yanayojiri Aleppo, lakini bado kuna mapigano makali yanayohusisha muungano uliopwaya wa makundi mbalimbali yanayoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la ISIS katika mji wa Mossul nchini Iraq.

Hata wakifanikiwa lazima utazuka mvutano wa kugawana ‘keki ya mafanikio’ lakini bila kusahau kuwa taifa la China bado linatunisha misuli katika bara hilo likijitanua kijeshi katika bahari ya Kusini mwa Asia dhidi ya swahiba wa Marekani (Japan), pia nchi ya Ufilipino yenye Rais mtata (Rodrigo Dutetre) asiyechagua mhalifu na asiye na hatia katika kusafisha nchi yake.

Lakini pia barani Afrika kuna migogoro inayofukuta iliyovuka mwaka ukiwemo uchaguzi wa hivi karibuni nchini Gambia, ambako Rais aliyeshindwa, Yahya Jammeh, hataki kuachia madaraka pia kuna mvutano wa uchaguzi nchini DRC na tamaa ya Pierre Nkuruzinza kujigeuza Rais wa maisha nchini Burundi, bila kusahau mzozo wa Serikali ya Ethiopia dhidi ya Waoromo.

Ni baadhi ya migogoro inayotarajiwa kuendelea kuigubika dunia huku ufumbuzi wake ukiwa mbali kama ilivyo kutoka ardhini kwenda mbinguni!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles