25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

11 Yanga wamshusha presha Pluijm

Hans-Van-De-PluijmNA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amechekelea hatua ya kurejea kikosini kwa nyota wake waliokuwa kwenye timu za Taifa zilizoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia, ambapo amedai sasa ndoto ya kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inaweza kutekelezeka.

Kurejea kwa nyota hao kumesaidia kumshusha presha Pluijm, ambaye awali alidai kuwa michuano hiyo imemtibulia mipango yake kutokana na mikakati aliyojiwekea ya kuhakikisha anawapa wachezaji wake programu ya pamoja ili waendane na kasi ya Ligi Kuu.

Jumla ya wachezaji 11 wa Yanga walikuwa kwenye timu za Taifa, ambapo wanne kati yao waliokuwa katika kikosi cha Zanzibar Heroes tayari wameungana na wenzao mazoezini, lakini wale wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ wanatarajia kuanza kujifua leo.

Zanzibar Heroes ambayo ilipangwa Kundi B katika  michuano hiyo, iliondoshwa kwenye kinyang’anyiro hicho hatua ya makundi, lakini Kili Stars ilitupwa nje hatua ya robo fainali na wenyeji Ethiopia na kikosi hicho kilirejea nchini juzi.

Kocha huyo raia wa Uholanzi aliliambia gazeti hili jana kuwa, amefarijika kwa hatua hiyo, kwani sasa kikosi chake kitakamilika na ataendelea kuwapa wachezaji wake programu aliyoandaa kuhakikisha wanaendeleza ushindani kwenye ligi iliyopangwa kuendelea Desemba 12, mwaka huu.

Wachezaji wa Zanzibar Heroes ambao tayari wameanza mazoezi Yanga ni mabeki Mwinyi Haji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, kiungo Said Makapu na mshambuliaji Matheo Simon.

Aidha, Mholanzi huyo alisema baadhi ya wachezaji vijana wenye umri chini ya miaka 20, waliokuwa wakifanya mazoezi na timu hiyo watapata nafasi ya kuendelea, ingawa bado anatafakari majina atakaowapa fursa hiyo.

“Nilichagua wachezaji tisa kutoka kikosi B cha Yanga ili niwaunganishe kwenye programu yangu ya mazoezi wakati nawasubiri wengine waliopo kwenye michuano ya Chalenji, lakini inawezekana baadhi yao wakabaki, licha ya kikosi kukamilika,” alisema.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo kwa kufikisha pointi 23, wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja nyuma ya vinara Azam FC, waliopo kileleni kwa kujikusanyia pointi 25.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles