27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi 941 wilayani Kibiti wakumbwa na homa ya mapafu

Na Gustafu Haule, Pwani

Wakazi 941 wa Halmashauri ya  Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani wamekumbwa na mlipuko wa  ugonjwa wa mapafu katika kipindi cha mwaka 2020.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba, ametoa taarifa hiyo juzi wakati akizungumza na Waandishi Habari ofisini kwake kuhusu namna ya kupambana na magonjwa ya milipuko.

Dk. Kamba amesema ugonjwa wa mapafu ni ugonjwa wa mlipuko na chanzo chake ni kirusi cha Influenza ambacho huingia katika mwili wa binadamu na kushambulia mapafu.

Amesema virusi wa Influenza ni moja kati ya wadudu hatari wanaosababisha ugonjwa huo kwa haraka na kwamba wasipochukuliwa hatua za haraka wanaweza kuleta madhara makubwa katika jamii.

Kamba amesema kuwa baada kubaini ugonjwa huo walichukua hatua za haraka na kufanikiwa kudhibiti ili usilete madhara zaidi huku akisema mpaka sasa wananchi waliokumbwa na ugonjwa huo wapo salama.

Kamba amesema ugonjwa wa mapafu huambukiza kama ilivyokuwa ugonjwa wa corona lakini njia pekee ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo ni mgonjwa kujitenga na jamii inayomzunguka.

“Mwaka jana ulitokea ugonjwa wa mlipuko wa homa ya mapafu huko Wilaya ya Kibiti na watu 941 waliambukizwa lakini ofisi yangu kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri husika tulifanikiwa kuudhibiti,”amesema Dk.Kamba.

Aidha, Dk. Kamba ametoa tahadhari kwa wananchi kuwa wawe makini pale wanapoona dalili tofuati za mwili na kwamba ni vyema wakajitokeza katika vituo vya afya vilivyopo karibu yao ili kufanya uchunguzi wa afya zao.

“Mkoa wa Pwani tumejipanga kikamilifu kukabiliana na magonjwa ya milipuko na kwasasa tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na magonjwa hayo kwakuwa lengo letu wananchi wawe salama,”amesema.

Hata hivyo, Dk. Kamba amewataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana vyema na maafisa afya wanaopita katika maeneo yao ili waweze kupewa elimu ya namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo, mwishoni mwa mwaka jana alimueleza Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima kuwa ugonjwa wa homa  ya mapafu ulitokea Wilaya ya Kibiti uliathiri nguvu kazi ya Taifa.

Aidha, Ndikilo ameshukuru timu ya wataalamu wa afya ya Mkoa wa Pwani ambayo ilishirikiana kwa karibu kudhibiti ugonjwa huo na kwamba mpaka sasa mkoa wake upo salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles