DAMIAN MASYENENE, MWANZA
MSAFARA wa kikosi cha Yanga umetua jana Mwanza kwa ndege asubuhi na kupokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wake, wakiongozwa na wanachama wa Tawi la Yanga Mjini.
Yanga inatarajia kucheza na Mbao kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, tayari kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo kutokana na rekodi mbaya kwa timu hiyo kutofunga katika Uwanja wa CCM Kirumba na Mbao.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya timu yake, Zahera alisema rekodi wanayojivunia Mbao kutofungwa na Yanga katika Uwanja wa CCM Kirumba wataisahau kesho, kwani Yanga imekuja kamili kuhakikisha inaibuka na ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya watani zao Simba.
Zahera alisema rekodi iliyopo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, haiwezi kuwatisha kwani hizi ni zama mpya na kikosi chake kinahitaji ushindi kwa namna yoyote.
“Kikosi changu kiko vizuri hakuna shida yoyote, tunaenda kupumzika na jioni tutaanza mazoezi, bado hatujajua eneo tutakalofanyia mazoezi, tunaendelea na mipango ya kutafuta uwanja wa mazoezi.
“Mambo ya rekodi ya kutoshinda Mwanza haiwezi kututisha, hii ni mara ya kwanza nakuja nadhani kwa namna tunavyokuja tutashinda, mambo ya zamani ni zamani hayo yamepita mimi sihofii rekodi za nyuma,” alisema.
Zahera aliwataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kesho kuishangilia timu yao iweze kuibuka na ushindi katika mchezo huo na kuzidi kuweka matumaini makubwa ya kubeba ubingwa msimu huu.
Yanga inashika usukani kwenye msimamo wa ligi, wakijikusanyia pointi 58 kati ya mechi 24 walizocheza, wakishinda 18, kutoa sare nne huku wakipoteza miwili.
Katika mchezo huo, Yanga itawakosa kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na beki wa kulia, Gadiel Michael, kutokana na kukabiliwa na adhabu ya kadi tatu za njano.