29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Malkia wa tembo jela miaka 17

Raia wa China, Yang Feng Glan ‘Malkia wa Meno ya  Tembo’ akishuka kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 17 na wenzake wawili. Picha na Imani Nathaniel

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewatia hatiani na kuwahukumu kwenda jela miaka 17, Malkia wa Meno ya  Tembo, Yang Feng Glan na wenzake wawili.

Washtakiwa hao walihukumiwa jana baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliitolewa na upande wa Jamhuri uliothibitisha makosa bila kuacha shaka.

Akitoa adhabu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alisema hasara iliyoingizwa na washtakiwa kwa Taifa ni kubwa na kwamba maliasili zipo kwa ajili ya kunufaisha watu wote na si mtu mmoja mmoja.

“Mshtakiwa wa kwanza Salvius Matembo na Philemon Manase mmekuwa wasaliti wa ndugu zenu, mmemua kula wenyewe kizani, mshtakiwa wa tatu, Yang umekaribishwa vizuri ukaamua kutumia vibaya nafasi hiyo.

” Kwa Makosa hayo na athari zilizoonyeshwa mahakama inatoa adhabu ifuatayo…kosa la kwanza, mshtakiwa wa tatu Yang utatumikia kifungo kisichopungua miaka 15 jela,

kosa la pili kwa mshtakiwa Matembo na Manase mtatumikia kifungo cha miaka isiyozidi miaka 15 na kosa la tatu kwa washtakiwa wote, mtakwenda jela miaka miwili ama kulipa faini mara mbili ya thamani ya meno ya tembo,”alisema.

Hakimu Shaidi alisema shamba la Muheza Tanga pamoja na nyumba ya mshtakiwa wa pili vilitokana na uhalifu huo hivyo vinarudi kwa wenyewe, vinataifishwa na kuwa mali ya Serikali.

“Washtakiwa walionyesha dharau kutumia malori ya Serikali kubebea meno ya tembo kupeleka bandarini, maelezo yao wakati wakihojiwa yalithibitisha kuhusika kwao katika biashara hiyo,” alisema Hakimu.

Kabla ya kufikia hatua hiyo Wakili wa Serikali, Salim Msemo aliomba washtakiwa wapewe adhabu kali na Shamba pamoja na nyumba iliyopo itaifishwe.

Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko aliomba adhabu watakayopewa izingatie miaka ambayo walikaa gerezani ambayo ni mitano.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni raia wa China, Yang Feng Glan (66), Salvius Matembo na Philemon Manase,

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 13 kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014.  Wanadaiwa kufanya biashara ya meno ya tembo 860 ambayo ni sawa na tembo 430 yenye thamani ya Sh 13,932,000,000.

Hakimu Shaidi alisema mashahidi wa Jamhuri walikuwa 11 na katika ushahidi wao shahidi wa saba alidai mshtakiwa wa pili Manase alikuwa akitumia Noah kubeba meno ya tembo kupeleka kwa Yang ambaye alikuwa akitumia Pick-up.

Inadaiwa waling’oa maua na kuficha meno ya tembo na kuna wakati shahidi huyo alihamishiwa Tangi Bovu kulinda kontena la futi 40 ambapo mshtakiwa wa pili alimuelekeza kuweka meno humo.

Shahidi mwingine ambaye ni dereva teksi alieleza jinsi alivyokuwa akitumwa Tanga mara nyingi kubeba meno ya tembo, na aliipeleka Mahakama hadi katika shamba la mshtakiwa wa pili ambapo walikuwa wakifukia meno hayo na kuyafukua wanapotaka kusafirisha kuja Dar es Salaam.

Inadaiwa meno hayo yalikuwa pia yakisafirishwa na malori ya Serikali kwenda Bandarini.

Shamba la Tanga lilikuwa limepandwa pilipili akidai kwamba shamba la mwekezaji wakati mazingira hayaashirii huo uwekezaji.

Shahidi Kiza Baraga kutoka Maliasili na Utalii alidai ujangili unaathari kubwa, wanyama wanaondoka, Taifa linapoteza mapato na silaha nyingi zinaingizwa kwa ajili ya mauji ya tembo.

Anadai silaha zinazotumika kuua tembo ni bunduki za kivita na riffle na kwamba tembo aliyeuawa na jangili hukutwa akiwa hana meno.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaotoa kwani bila ushirikiano wa wananchi wasinhefanikiwa.

Pia aliishukuru Mahakama kwa adhabu waliyotoa kwa mujibu wa sheria, ameshukuru mawakili wa pande zote mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles